Presha kwa Amorim mashetani wekundu wakiumwa na nyuki wa Brentford
LONDON, Uingereza
SHINIKIZO zinaendelea kumwandama Ruben Amorim baada ya Manchester United kupoteza 3-1 dhidi ya Brentford kwenye Ligi Kuu hapo Septemba 27, 2025.
Kipigo hicho kinamweka tena kocha huyo kutoka Ureno katika darubini zaidi baada ya juhudi zake za kupata ushindi wa pili mfululizo ligini kugonga mwamba.
Matumaini ya United ya kugeuza mchezo yalikuwa mikononi mwa Bruno Fernandes, lakini nahodha huyo aliona penalti yake katika kipindi cha pili ikipanguliwa na Caoimhin Kelleher baada ya kusubiri zaidi ya dakika nne kutokana na uamuzi wa VAR ili kubaini iwapo Nathan Collins alistahili kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumnyima Bryan Mbeumo nafasi ya wazi ya kufunga bao.
Hata hivyo, refa Craig Pawson hakubadilisha uamuzi wake wa kumpa Collins kadi ya njano, licha ya video kuonyesha wazi kwamba beki huyo hakufanya jaribio lolote la kucheza mpira alipomvuta mchezaji mwenzake wa zamani Mbeumo.
Tukio hilo liligeuka kuwa uamuzi muhimu, kwani United haikufanikiwa kujinasua tena. Hali yao iliendelea kuwa mbaya zaidi katika muda wa nyongeza baada ya Mathias Jensen kufunga bao tamu la tatu lililohakikisha ushindi wa Brentford na kuhakikishia United kichapo cha tatu katika michuano minne ya mwisho ugenini London Magharibi. Ushindi wao wa wiki jana dhidi ya Chelsea ulifutika kwa mchezo dhaifu.
Brentford ya kocha Keith Andrews ilipiga hatua mapema kupitia mabao mawili ya haraka ya Igor Thiago ndani ya dakika 20 za kwanza.
Benjamin Sesko alifunga bao lake la kwanza kambini mwa United na kupunguza mwanya, lakini vijana wa Amorim hawakuonekana thabiti katika jaribio lao la kurejea mchezoni.
Penalti ya pili aliyokosa Fernandes msimu huu ilionyesha wazi walivyopoteza nafasi muhimu.
Kipigo hicho kimeiacha United bila ushindi katika mechi nane mfululizo ya ugenini ya ligi na kuisukuma hadi nusu ya chini ya jedwali katika nafasi ya 14.
Brentford nao waliwaruka United na kutulia nafasi ya 13 baada ya kupata alama tatu walizostahili.
Baada ya mechi, Amorim alikiri kufadhaishwa na uamuzi dhidi ya Collins, lakini akasema vijana wake walipaswa kuwa na utulivu na nidhamu zaidi baada ya Fernandes kushindwa kufunga.