Dimba

Riadha za Dunia: Kipyegon aongoza Wakenya kutinga nusu-fainali ya 1,500m

Na GEOFFREY ANENE September 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wote wanne – Faith Kipyegon, Nelly Chepchirchir, Susan Ejore na Dorcus Ewoi – walifuzu Jumamosi kushiriki nusu-fainali ya mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan.

Bingwa mtetezi Kipyegon alitawala Kundi la Nne akimaliza kwa dakika 4:02.55 akifuzu pamoja na Sarah Madeleine (Ufaransa), Sarah Healy (Ireland) na Marta Zenoni (Italia).

Chepchirchir alishinda Kundi la Pili kwa 4:07.01, huku Ejore na Ewoi wakifuzu kupitia Kundi la Tatu na kwanza kwa 4:01.99 na 4:04.93, mtawalia. Nusu-fainali zitaandaliwa Septemba 14 saa tisa alasiri.

Faith Kipyegon (kulia) mbele ya Laura Muir wa Uingereza na Marta Zenoni wa Italia katika mchujo wao. PICHA | REUTERS

Kenya ilipata afueni baada ya kutokuwepo kwa Diribe Welteji wa Ethiopia, mmoja wa wapinzani wakubwa wa Kipyegon. Welteji alisimamishwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baada ya Kitengo cha Maadili ya Riadha (AIU) kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Ethiopia kumwachia huru kwa kosa la kukataa kutoa sampuli ya uchunguzi. Kupigwa marufuku kwa muda kulimnyima nafasi ya kushiriki mashindano.

Welteji aliyeshinda fedha ya 1,500m kwenye Riadha za Dunia mjini Budapest 2023, anashikilia nafasi ya tatu duniani nyuma ya Kipyegon na Gudaf Tsegay. Katika 800m, Welteji yuko nafasi ya 24 duniani. Kutoshiriki kwake kunaipa Kenya nafasi bora zaidi katika 1,500m.

Licha ya kushiriki mashindano machache msimu huu, Kipyegon aliingia Tokyo kama kipenzi cha mashabiki. Amevunja rekodi za dunia za maili moja na 1,500m mwaka huu, na kushikilia muda wa tatu-bora kihistoria katika 1,000m.

Medali kochokocho

Staa huyo ana medali tatu za dhahabu za Olimpiki katika 1,500m na hajapoteza mbio hiyo kwa miaka minne. Ushindi Tokyo utamfanya afikie rekodi ya mwanamume Hicham El Guerrouj kutoka Morocco, bingwa pekee wa dunia mara nne katika 1,500m.

Pia, mpinzani mwingine mkubwa, Tsegay, aliamua kuzingatia 5,000m na 10,000m kutokana na ratiba kugongana, huku Beatrice Chebet wa Kenya pia akichagua 5,000m na 10,000m.

Hiyo inaacha Kipyegon akiwa na njia wazi zaidi ya taji, ingawa Jessica Hull (Australia), Freweyni Hailu (Ethiopia) na Chepchirchir wameonyesha ni wapinzani halisi. Chepchirchir alishinda mashindano kadhaa ya Diamond League msimu huu ikiwemo fainali mjini Zurich, Uswisi.

Mary Moraa (pili kulia) amaliza nyuma ya Helena Ponette wa Ubelgiji mchujo wa 4x400m mseto Jumamosi. Moraa atashiriki pia kitengo cha 800m. PICHA | REUTERS

Katika 800m, Kenya inawakilishwa na bingwa mtetezi Mary Moraa pamoja na Lilian Odira, Sarah Moraa na Vivian Kiprotich. Odira, namba nne duniani, anaipa Kenya nguvu zaidi, ingawa upinzani mkali unatarajiwa kutoka kwa Keely Hodgkinson (Uingereza) na Audrey Werro (Uswisi).

Kwa kutokuwepo Welteji na Tsegay, Kenya inaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kuongeza medali kupitia Kipyegon na Chepchirchir kwenye 1,500m, huku Moraa akilenga kutetea taji la 800m.