Sesko akaribia kuhamia Manchester United
BENJAMIN Sesko wa klabu ya RB Leipzig amesema yuko tayari kujiunga na Manchester United hata baada ya klabu hiyo kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mshambuliaji huyo mahiri wa timu ya taifa ya Slovenia amekuwa kwa rada ya Manchester United, huku ikiripotiwa kwamba kocha Ruben Amorim anataka huduma yake kuongeza makali kwenye safu ya ushambuliaji kwa ajili ya msimu ujao wa 2025/2026.
Ili kumnasa nyota huyo mwenye umri wa miaka 22, Manchester United wamekubali kutoa Sh12.6 bilioni ambazo zimeitishwa na Leipzig.
Ujio wake unatarajiwa kumaliza shida ya kocha Amorim ambaye amekuwa akitafuta namba 9 kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, baada ya hapo awali kuwasajili Matheus Cunha kutoka klabu ya Wolves kwa mkataba uliogharimu Sh10.7 bilioni.
Amorim alielekeza akili zake kwa Sesko baada ya Aston Villa kukataa kumuachili Ollie Watkins. Tayari mkurugenzi wa masuala ya usajili katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Christopher Vivell amesema makubaliano kati ya pande zote yanakaribia kukamilika.
Afisa wa kusimamia mazungumzo hayo, Matt Hargreaves aliongoza ujumbe kutoka Old Trafford kwenda nchini Ujerumani kuweka mazungumzo hayo kwenye hatua nzuri.
Vivell alikuwa mfanyakazi katika kampuni ya Red Bull inayozimiliki klabu za Leipzig na timu ya zamani ya Sesko, Salzburg kwa miaka saba na amemtaja nyota huyo kuwa miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu watakaokuja kuwa wakali zaidi siku za usoni.
“Namfahamu vizuri. Ana kila kitu cha kumfanya awike zaidi siku zijazo. Mbali na kuwa fundi hodari, ni mwepesi, mwenye uwezo mkubwa kuwania mpira hata ukiwa hewani na ni mfungaji mahiri asiyekaa sehemu moja uwanjani.”
Awali kabla ya kumnasa Viktor Gyokeres, Sesko alikuwa kwenye orodha ya kocha Mikel Arteta wa Arsenal ambayo ingempa fursa ya kucheza kwenye Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya, lakini amechagua kujiunga na Manchester ambao walimaliza katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa EPL, mbali na kumaliza msimu bila chochote.
Vile vile matumaini ya kocha Eddie Howe wa Newcastle United yameambulia patupu baada ya nyota aliyefunga mabao 39 kwa misimu miwili kwenye Ligi Kuu ya Bundesliga kukataa kuyoyomea St James’ Park mjini Westminister.