Kila mchezaji wa Harambee Stars kutia mfukoni Sh1 milioni kwa ushindi dhidi ya DRC
WACHEZAJI wa Harambee Stars wamejihakikishia Sh1 milioni mfukoni kwa ushindi mechi yao ya ufunguzi dhidi ya DRC. Hii ni kwa mujibu wa ahadi ya Rais William Ruto kuwatia motisha kufana kwenye dimba la CHAN.
Rais William Ruto alipoandalia kikosi cha Harambee Stars kifungua kinywa katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi Jumamosi alitangaza pesa watakazopata kutokana na ufanisi wao kwenye michuano ya CHAN.
Harambee Stars ambao wamepangiwa Kundi A wamekalifisha DR Congo katika uwanja wa Kimataifa wa MISC, Kasarani, Jumapili, Agosti 3, 2025.
Wakati wa karamu hiyo ya kifungua kinywa, Rais aliandamana na Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, Katibu wa Kudumu kwenye wizara hiyo, Elijah Mwangi na mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uandalizi wa mashindano hayo, Nicholas Musonye pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu Serikalini.
Wakati wa ziara hiyo, Rais aliahidi motisha za ukarimu ambazo ni: Sh1 milioni kwa kila mchezaji kwa ushindi, Sh500,000 kwa matokeo ya sare. Aidha timu nzima itapokea jumla ya Sh60 milioni iwapo itafuzu kwa robo fainali, Sh70 milioni kwa kutinga nusu fainali na Sh600 milioni iwapo watatwaa ubingwa.
Akitoa ahadi hizo, Rais Ruto alitoa mwito kwa Wakenya wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo ambayo pia itakabiliana na Angola, Morocco na Zambia katika mechi zake ambazo zitachezewa katika uwanja huo wa kimataifa ulio na uwezo wa kusitiri zaidi ya mashabiki 48,000.