Shabana tabasamu tu baada ya vifaa vyao muhimu kurejea
KOCHA wa Shabana, Peter Okidi ana imani sasa timu yake itaanza kuandikisha matokeo mema baada ya wachezaji wake tegemeo kupona majeraha yaliyowaweka mkekani kwa kipindi kirefu.
Kulingana na Okidi, baadhi ya sababu zilizochangia timu yake kudondosha alama, hasa inapocheza nyumbani, ni kukosekana kwa wachezaji wake stadi Brian Michira, George Orako, Justice Omwando na Keith Imbali.
Akizungumza juzi baada ya kuiongoza Tore Bobe kula sare tasa na miamba Gor Mahia ugani Gusii, Okidi alisema urejeo wa wachezaji hao utaipiga jeki timu hiyo yenye makazi yake mjini Kisii na kuwawezesha kutimiza malengo yao msimu huu.
“Kurejea kwa wachezaji hawa ni motisha kwa kikosi kizima. Walipata majeraha wakati tulikuwa tunawahitaji sana na wamepona wakati tunawahitaji hata zaidi,” Okidi alidokeza.
Wachezaji hao wamekuwa mhimili mkubwa kwa Shabana kwani wanapokuwa uwanjani, timu hiyo huandikisha matokeo ya kuridhisha.
Mbali na Orako ambaye ni beki, Omwando, Imbali na Michira wamekuwa wakiimarisha safu ya kati na mashambulizi ya Tore Bobe.
Michira ndiye mfungaji bora wa Shabana na amefanikiwa kuona lango la wapinzani mara nne.
Alijeruhiwa mnamo Oktoba 5, 2025 katika mchezo wa nne wa ligi walipomenyana na Tusker FC ugani Kasarani.
Mechi hiyo iliisha sare ya 1-1. Alirejea hivi maajuzi kutoka mkekani na kupewa dakika chache wakati Shabana walipoteza 3-1 dhidi ya Nairobi United.
Michira alitangaza kurejea kwake kwa kufanya bao hilo la pekee la Shabana kupitia mkwaju wa penalti. Vile vile katika mchezo wa juzi dhidi ya Gor Mahia, Michira aliingizwa katika kipindi cha pili.
“Kurejea kwa wanne hawa ni sawia na sisi kufanya usajili wa wachezaji katika dirisha dogo,” Okidi alisema.
Kocha huyo aliwapa wanne hao changamoto ya kushirikiana na wenzao kikosini ili kuhakikisha kuwa wanafikisha kikomo mazoea ya timu hiyo kupoteza mechi za nyumbani.
Kati ya mechi 16 ilizozicheza, Shabana imepoteza mechi nne na zote zimetokea wakicheza mbele ya mashabiki wao wanaofika kwa fujo kuwashabikia.
“Lazima tuvunje kasumba hiyo ya kutoshinda Gusii. Tulielewana na wachezaji kuwa kutoka sasa kwenda mbele, hakuna kupoteza mechi nyumbani,” Okidi alisema.
Baada ya kuandaa gozi lao na Gor Mahia kwa amani kinyume na ilivyokuwa mwaka jana na matarajio ya wengi, Tore Bobe itawaalika Sofapaka mwishoni wa wiki hii ugani Gusii.
Shabana kwa sasa inashikikia nafasi ya nne katika Ligi na alama 24. AFC Leopards, inaongoza msururu wa jedwali kwa alama 30, tatu mbele ya namba mbili Gor Mahia, ambao wana mchezo mmoja mkononi na mwingine ambao uamuzi unasubiriwa kutolewa kufuatia uni.
Kakamega Homeboyz wako katika nafasi ya tatu kwa alama 24, sawia na Shabana lakini wana tofauti nzuri ya mabao dhidi ya wapinzani hao.