Dimba

Shujaa yateleza raga za Hong Kong 7s, lazima ipige Ufaransa

Na GEOFFREY ANENE March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA Shujaa imejiweka pabaya baada ya kuandikisha matokeo mseto katika mechi zake mbili za Kundi C kwenye duru ya Raga za Dunia ya Hong Kong Sevens, Ijumaa.

Vijana wa kocha Kevin Wambua, ambao wako katika mduara hatari wa timu nne za mwisho, walianza mawindo yao kwa kishindo baada ya kuzamisha Uhispania kupitia miguso ya Patrick Odongo, George Ooro na Samuel Asati na mikwaju ya Nygel Amaitsa.

Uhispania, ambao ni nambari mbili kwenye ligi hiyo ya mataifa 12, waliponzwa na penalti tano katika kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Wakenya walijikwaa katika mechi ya pili licha ya kuianza vyema baada ya Odongo kutinga mguso ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Amaitsa.

Uingereza ilisawazisha 7-7 kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika na kisha kuvuna ushindi ilipopata mguso wake wa pili katika kipindi cha pili.

Great Britain, ambayo iliingia Hong Kong Sevens ikikamata nafasi ya nane, ilijikatia tiketi ya robo-fainali baada ya kupiga Kenya kwani ilikuwa imezaba Ufaransa 12-7 katika mechi yake ya kwanza.

Kenya sasa lazima ipepete mabingwa wa Olimpiki, Ufaransa hapo Jumamosi asubuhi (5.16am) ili kunyakua tiketi moja iliyosalia ya robo-fainali kutoka kundi hilo.

Vijana wa kocha Wambua wanapigana kuepuka kusukumwa katika mashindano ya kuwania kusalia kwenye Raga za Dunia 2025-2026 dhidi ya timu zinazotaka kupandishwa ngazi kutoka Challenger Series.

Shujaa imerejea kwenye Raga za Dunia msimu huu wa 2024-2025 baada ya kuwa nje mwaka mmoja.