Dimba

Si kuzuri kambini Emirates matumaini ya kufukuzia mataji yakiyeyuka ghafla

Na CHRIS ADUNGO January 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

PAMOJA na ongezeko la visa vya majeraha, kusuasua kwa Arsenal katika mechi tatu zilizopita kunatarajiwa kumzidishia Mikel Arteta presha ya kusajili mvamizi wa haiba kubwa mwezi huu licha ya kocha huyo raia wa Uhispania kusisitiza kwamba kikosi chake hakihitaji mchezaji mpya kwa sasa.

Manchester United waliendeleza masaibu ya Arsenal mnamo Jumapili kwa kuwabandua katika raundi ya tatu ya Kombe la FA ugani Emirates. Licha ya kusalia uwanjani na wachezaji 10 pekee kwa zaidi ya saa moja, Red Devils walifunga wenyeji wao penalti 5-3 kufuatia sare ya 1-1 baada ya muda wa ziada.

Ingawa Arsenal walitamalaki mechi hiyo, walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Declan Rice na Kai Havertz aliyeshindwa kufunga penalti. Awali, nahodha Martin Odegaard naye alipoteza mkwaju wa penalti katika kipindi cha pili, dakika tisa baada ya beki Diogo Dalot wa Man-United kuonyeshwa kadi nyekundu.

SOMA PIA: Arsenal nje Kombe la FA, ‘mashetani wekundu’ Man United wakisherehekea kusonga mbele

Arsenal sasa wameaga Kombe la FA katika raundi ya tatu kwa mara ya tatu katika misimu minne iliyopita. Hadi waliposhuka dimbani Jumapili, walikuwa wameambulia sare ya 1-1 dhidi ya Brighton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugenini na kukubali kichapo cha 2-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Carabao Cup dhidi ya Newcastle United nyumbani. Mechi dhidi ya Man-United ilikuwa ya pili kati ya tano mfululizo ambazo Arsenal watatandaza nyumbani mwezi huu.

Vijana hao wa kocha Mikel Arteta wataalika Tottenham Hotspur Jumatano kwa gozi kali la London Kaskazini katika EPL kabla ya kuvaana na Aston Villa kisha kupepetana na Dinamo Zagreb ya Croatia katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Watafunga kampeni zao za Januari kwa michuano miwili ya ugenini dhidi ya Wolverhampton Wanderers na Girona katika EPL na UEFA mtawalia.

Kichapo kutoka kwa Newcastle mnamo Januari 7 kiliwaweka Arsenal guu moja nje ya kipute kingine muhimu msimu huu. Miamba hao wataanza Februari kwa mtihani mgumu wa EPL dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City ugani Emirates kabla ya kurudiana na Newcastle katika nusu-fainali ya Carabao Cup ugani St James’ Park. Lazima washinde pambano hilo kwa angalau mabao 3-0 ili watinge fainali dhidi ya Liverpool au Tottenham Hotspur.

Hadi kufikia wikendi iliyopita, Kombe la FA ndilo la pekee lililotarajiwa kuwapa Arsenal nafasi murua zaidi ya angalau kujizolea taji muhula huu.

SOMA PIA: FA: Opta inasema Arsenal kichwa dhidi ya Man U, lakini historia yaonyesha yeyote anaweza

Sasa matumaini yao ya kufukuzia makombe manne msimu huu, likiwemo taji la Carabao Cup, yameyeyuka ghafla.

Isitoshe, ndoto ya kunyanyua ubingwa wa EPL na ufalme wa UEFA imedidimia ikizingatiwa ukosefu wa uthabiti wa kikosi chao baada ya wanasoka Bukayo Saka, Gabriel Jesus, Ethan Nwaneri, Ben White na Takehiro Tomiyasu kupata majeraha yatakayowaweka mkekani kwa muda mrefu.

Kufikia sasa, Arsenal wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa pointi 40, sita nyuma ya viongozi Liverpool ambao wana pambano moja zaidi la akiba.

Aidha, wanashikilia nafasi ya tatu kwenye UEFA kwa alama 13 baada ya kushinda mechi nne, kupiga sare mara moja na kupoteza mchuano mmoja kati ya sita iliyopita.

Japo hawako vibaya sana kwenye vipute hivyo viwili, huenda wakashindwa kuhimili ushindani mkali iwapo watakosa kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho na kujinasia huduma za fowadi matata atayaweka Havertz katika ulazima wa kusugua benchi.

SOMA PIA: Kipigo cha Arsenal mikononi mwa Newcastle chaambia Arteta anahitaji straika

Mechi ya Jumapili ilikuwa ya pili kukutanisha Arsenal na Man-United katika kipindi cha takriban wiki tano zilizopita. Watani hao wakuu sasa wamekutana mara 242 na Arsenal wameshinda mara 90, Man-United wakatamba mara 102 huku michuano 50 ikikamilika kwa sare.

Kabla ya Jumapili, pambano la mwisho kati ya miamba hao lilikuwa la EPL mnamo Desemba 4, 2024 ambapo Arteta aliongoza waajiri wake kuvuna ushindi wa 2-0 ugani Emirates. Mechi hiyo ilikuwa ya nne kwa mkufunzi Ruben Amorim kusimamia kambini mwa Man-United.

Tofauti na Arsenal, Man-United watashuka dimbani kwa mechi yao ijayo ya EPL dhidi ya Southampton wakiwa na motisha tele. Hadi walipodengua Arsenal kwenye Kombe la FA, mabingwa hao mara 20 wa EPL walikuwa wametoka nyuma na kulazimishia Liverpool sare ya 2-2 ligini katika uwanja wa Anfield mnamo Januari 5.

Mapambano yao mawili yaliyopita yamekuwa onyesho kamili la ukomavu na ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa makali ya Red Devils chini ya Amorim.