South Coast Pirates, Mwamba, Strathmore, Nakuru na Impala roho mkononi siku ya mwisho ya Kenya Cup
MSIMU wa kawaida wa Ligi Kuu ya raga ya wanaume ya wachezaji 15 kila upande 2024-2025 utakamilika leo.
Impala, Nakuru, Strathmore Leos, Kisumu, Mwamba na South Coast Pirates kila moja itatumai kuponea kutemwa.
Pirates kutoka Kaunti ya Kwale wako pabaya zaidi kushushwa daraja katika msimu wao wa kwanza kabisa kwenye ligi hiyo maarufu kama Kenya Cup. Vijana hao wa kocha Kelvin Amiani wanakamata mkia kwa alama tisa kwenye ligi hiyo klabu 12.
Pirates wanahitaji ushindi pekee wa alama ya bonasi dhidi ya nambari tatu Menengai Oilers ili kuepuka kuangukiwa na shoka. Usalama wao pia utategemea matokeo ya nambari nane Nakuru (alama 14), nambari tisa Strathmore (13), nambari 10 Kisumu (13) na nambari 11 Mwamba (12).

Ina maana kuwa Pirates wanahitaji muujiza dhidi ya Oilers ili kuponea kushushwa ngazi. Mwamba lazima wapige Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ili kujihakikishia usalama.
Hata hivyo, Mwamba bado wanaweza kuepuka kushushwa ngazi wakipata sare naye mmoja kati ya Strathmore na Kisumu apepetwe. Strathmore wanaalika nambari tano Kenya Harlequin maarufu Quins mtaani Madaraka nao Kisumu ni wenyeji wa washindi wa mataji mengi ya Kenya Cup, Nondescripts maarufu Nondies.
Timu mbili za mwisho baada ya mechi za raundi ya 11 (mwisho) zitatupwa katika Ligi ya Daraja la Pili kujaza nafasi ya mbili zitakazopandishwa ngazi.
Kwa sasa, vita vya kupanda daraja vinahusisha timu za wanafunzi wa vyuo vikuu vya Masinde Muliro (Mmust), Daystar Falcons, Catholic Monks, Zetech Oaks, JKUAT Cougars na ‘madeejay’ wa Homeboyz wanaofuatana kutoka nafasi ya kwanza hadi sita, mtawalia.
Mmust na Daystar wako nusu-fainali kwa kumaliza msimu wa kawaida katika nafasi mbili za kwanza. Monks, Zetech, JKUAT na Homeboyz watashiriki mechi za muondoano ili kupata tiketi mbili zilizosalia za nusu-fainali.
Ratiba ya Kenya Cup Jumamosi:
South Coast Pirates vs Menengai Oilers (3.00pm Seacrest Grounds Diani Kwale)
Strathmore Leos vs Kenya Harlequin (4.00pm Strathmore Sports Complex Nairobi)
Kabras Sugar vs KCB (3.00pm ASK Showground Kakamega)
Mwamba vs KU Blak Blad (4.00pm)
Kisumu vs Nondescripts (4.00pm ASK Showground Mamboleo)
Impala vs Nakuru (4.00pm Impala Grounds Nairobi)