Sportpesa yatangaza udhamini wa Sh15 milioni kwa National Sevens Circuit
Kampuni ya SportPesa imetangaza kuwekeza Sh15 milioni kwenye ligi ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande itakayofanyika Julai 26 hadi Septemba 14, 2025.
Kupitia fedha hizo, SportPesa itasalia kama mdhamini mkuu wa ligi hiyo ambayo itaendelea kufahamika kama SportPesa National Sevens Circuit.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo mjini Nairobi hapo Julai 23, Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga Kenya (KRU), Harriet Okatch, alishukuru SportPesa kwa kusimama na mchezo huo na kwa kukubali kuwa wadhamini wa ligi hiyo.
“Msaada wenu umekuja kwa wakati mzuri kabisa. Ligi hii ndio mwanzo wa safari yetu ya kufuzu kushiriki Ligi ya Daraja ya Juu kabisa duniani ya HSBC kwa timu zetu za wanaume na wanawake mwaka ujao. Tuna imani kubwa kuliko hapo awali kuwa Kenya itarejea tena kwenye jukwaa hilo kuu,” akasema Okatch.
Willis Ojwang kutoka SportPesa alieleza kuwa kampuni hiyo imedhamiria kusaidia ukuaji na maendeleo ya michezo na vipaji vya humu nchini. “Kwa miaka mitatu mfululizo tangu tuingie kwenye ligi hii ya kitaifa, mashindano haya ambayo huchukua takriban miezi mitatu na kushirikisha zaidi ya klabu 50, yamekuwa chimbuko la vipaji vikubwa na vimekuwa chanzo cha wachezaji wa timu ya taifa ya Shujaa. Tunajivunia kwamba kupitia SportPesa Sevens, tuliiona timu iliyotwaa ubingwa wa Kombe la Afrika mwaka 2023, kufuzu kwa Olimpiki, na kisha kurejea kwa kasi kwenye mfululizo wa HSBC 2024-2025,” akasema Ojwang.
Katika jumla ya Sh15, kuna migao mitatu. Sh3 milioni zitatolewa kwa klabu sita wenyeji (Mombasa SC, Nakuru RFC, Kenya Harlequin RFC, Embu RFC, Mwamba RFC na Kisumu RFC), Sh6 milioni zitagharamia matangazo ya moja kwa moja ya mashindano, na Sh2.3 milioni zitatumika kama zawadi ya pesa kwa kila duru pamoja na washindi wa jumla.
Akizungumza kwa niaba ya klabu zitakazokuwa wenyeji, Katibu wa Harlequin, Nekesa Were, alishukuru SportPesa na KBL kwa kusaidia maendeleo ya mchezo huu nchini. “Kwa klabu nyingi wenyeji, tunategemea ligi hiyo kugharamia mahitaji ya timu zetu wakati msimu wa raga ya wachezaji 15 kila upande unapoanza. Ndiyo maana tunatoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono mchezo huu,” akasema.
Nekesa pia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza raga ya wanawake humu nchini kwa kuhimiza klabu kuendelea kuunda na kukuza timu zao za wanawake.
Mgao wa tuzo ya washindi katika kila duru:
Daraja la juu
Mshindi Sh100,000
Nambari mbili Sh50,000
Nambari tatu Sh25,000
Daraja la pili
Mshindi Sh50,000
Wanawake
Mshindi Sh70,000
Nambari mbili Sh30,000
Tuzo ya ligi baada ya duru zote
Mshindi Sh300,000
Nambari mbili Sh150,000
Nambari tatu Sh100,000
Tarehe za ligi ya Sportpesa Sevens
Julai 26-27: Driftwood Sevens
Agosti 2-3: Prinsloo Sevens
Agosti 16-17: Christie Sevens
Agosti 23-24: Embu Sevens
Septemba 6-7: Kabeberi Sevens
Septemba 13-14: Dala Sevens