Ubashiri wasema Arsenal itamaliza ukame wa mataji ya Klabu Bingwa Ulaya
SIKU moja baada ya kulipua wapinzani wao wa karibu Bayern Munich 3-1 katika Wiki ya Tano hapo Novemba 26, 2025, Arsenal wanapigiwa upatu kushinda taji lao la kwanza kabisa la Klabu Bingwa Ulaya msimu 2025-2026.
Kompyuta ya Opta imewapa Arsenal uwezo wa asilimia 24.36 baada ya ushindi huo, wakiwa mbele kidogo ya mabingwa mara sita Bayern ambao wana asilimia 15.78.
PSG wako nafasi ya tatu na uwezo wa asilimia 12.67, huku Manchester City, Real Madrid na Chelsea wakiwa nafasi ya nne, tano na kwa asilimia 7.66, asilimia 7.09 na asilimia 5.84, mtawalia.
Barcelona (asilimia 5.34), Inter Milan (4.02), Liverpool (3.25), Atletico Madrid (2.84), Dortmund (2.72), Leverkusen (1.84) na Newcastle (1.83) pia ni miongoni mwa timu zilizopewa asilimia 1.00 au zaidi za kushinda Champions League.
Katika orodha ya timu Opta imebashiri zitafuzu moja kwa moja kushiriki raundi ya 16-bora ni Arsenal (asilimia 99.9), Bayern Munich (92.9), PSG (89.47), Real Madrid (84.76), Inter Milan (65.10), Manchester City (59.24), Chelsea (58.29) na Borussia Dortmund (52.47).
Timu zitakazokamilisha awamu hii ya ligi kati ya nambari tisa na 24 zitalazimika kushiriki awamu nyingine ili kuingia 16-bora.
Arsenal, ambao matokeo yao bora kwenye L;abu Bingwa Ulaya ni nambari mbili mwaka 2006, wanaendelea kudhihirisha si abiria, bali wagombea halisi wa taji baada ya kutoa onyo kali kwa kupita mtihani wa Bayern.
Ni mechi iliyokutanisha timu mbili kali zaidi barani Ulaya wakati huu uwanjani Emirates.
Kikosi cha Mikel Arteta, ambacho hakikupoteza mechi 15 mfululizo, kilikuwa kinakaribisha Bayern Munich waliokuwa wametawala michuano 17 kati ya 18 katika mashindano yote.
Kwa pamoja, vigogo hao wa Ulaya walikuwa wameshinda mipepetano 32 kati ya 36 msimu huu wa 2025-2026.
Lakini ni mmoja tu aliyeibuka na ushindi: Arsenal.
Wakati Bayern waliwasili ugani Emirates kama mashine kali zaidi ya kushambulia barani Ulaya, Arsenal waliingia katika uwanja wao kama ngome ya ulinzi.
Wanabunduki wa Arsenal walikuwa wamefungwa mabao 0.37 pekee kwa mechi katika mashindano yote, na takwimu ya 0.55 ya mabao yaliyotarajiwa dhidi yao ikiwa bora zaidi katika Ligi Tano Kubwa za Ulaya.
Bayern, kwa upande wao, walikuwa tayari wamesukuma nyavuni mabao 65, wastani wa mabao 3.4 kwa mechi, na hawakuwa wamefunga chini ya mabao mawili hata mara moja msimu huu.
Kwa dakika 45 za kwanza, ubora ulionekana. Kichwa kizuri kutoka kwa Jurrien Timber kilisawazishwa na bao la Lennart Karl, na mchuano ukawa sawa kati ya miamba wawili. Lakini kipindi cha pili kilimilikiwa moja kwa moja na Arsenal.
Mabadiliko ya Arteta yalisababisha mwelekeo mpya. Riccardo Calafiori alikimbia upande wa kushoto na kumpa Noni Madueke pasi iliyomtunuku bao lake la kwanza kwa klabu, na kuwasha moto Emirates.
Baadaye, Gabriel Martinelli alimaliza kwa ukatili shambulizi na kufanya ushindi wa 3–1 ambao ulionekana mkubwa zaidi ya matokeo.
Arsenal walipangua Bayern kwa mashambulizi ya aina nyingi ikiwemo tishio katika ikabu.
Walipiga makombora 10 kati ya 13 katika kipindi cha pili na kuzalisha 3.11 yaliyotarajiwa, kiasi kikubwa dhidi ya timu kama Bayern, ambayo haijawahi kuruhusu zaidi ya magoli matatu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Cha kuvutia zaidi, Arsenal walizima kabisa safu kali zaidi ya ushambuliaji barani Ulaya. Bayern walifyatua shuti nane tu, rekodi yao ya chini msimu huu.
Mvamizi matata Harry Kane hakutuma shuti hata moja, kwa mara ya kwanza katika historia yake dhidi ya Arsenal.
Baada ya mapumziko, Bayern waligusa mpira mara saba tu ndani ya kisanduku cha Arsenal.
Na yote hayo yalifanyika bila wachezaji watatu muhimu – Martin Odegaard, Gabriel Magalhaes na Viktor Gyokeres. Kina cha kikosi cha Arsenal sasa kimefika kiwango ambacho kila mabadiliko huongeza nguvu.
Huo ulikuwa mtihani mkubwa zaidi wa Arsenal msimu huu, na waliupita kwa kiwango cha juu. Vijana wa Arteta wanasalia timu pekee ambayo haijapoteza alama kwenye Klabu Bingwa Ulaya, ikiongoza ligi hiyo ya timu 36 kwa pointi 15. Arsenal pia wako mbele kwa pointi sita kwenye Ligi Kuu.
Kwa sasa, Arsenal wanaonekana kama timu bora zaidi duniani, na wanacheza kana kwamba wanajua hivyo.