Vroooom! Safari Rally yavutia madereva 39 ikiwemo mabingwa Ogier na Rovanpera
MADEREVA 39 wameingia raundi ya tatu ya Mbio za Magari Duniani (WRC), Safari Rally, itakayofanyika katika kaunti za Nairobi na Nakuru mnamo Machi 20-23, 2025.
Orodha ya washiriki ilitangazwa Ijumaa na inajumuisha madereva kutoka Kenya, Uingereza, Finland, Ubelgiji, Estonia, Japan, Ufaransa, Ireland, Ugiriki, Uswidi, Paraguay, Poland, Uhispania, Argentina, India, Tanzania na Uganda.
Mabingwa wa dunia Sebastien Ogier kutoka Ufaransa (mwaka 2013, 2014, 2015, 2016, 2017, 2018, 2020 na 2021), Kalle Rovanpera wa Finland (2022 na 2023), Ott Tanak kutoka Estonia (2019) na Mbelgiji Thierry Neuville (2024) pia wako katika orodha hiyo.

Timu ya magari ya Toyota ilitawala raundi mbili za kwanza msimu huu kupitia kwa Ogier akishirikiana na Vincent Landais kwenye Rallye Monte Carlo mjini Monaco, Ufaransa mnamo Januari 23-26. Namba mbili akawa Elfyn Evans kutoka Wales akielekezwa na Scott Martin nchini Uswidi. Totoya itakuwa ikifukuzia ushindi wa tano mfululizo kwenye WRC Safari Rally.
Evans anaongoza ligi hiyo ya raundi 16 kwa alama 61 baada ya kuanza msimu kwa kukamata nafasi ya pili mjini Monaco. Amefungua mwanya wa alama 28 dhidi ya mpinzani wa karibu Ogier naye Rovanpera pia kutoka Toyota anakamilisha tatu-bora kwa pointi 31.
Rovanpera ndiye bingwa mtetezi. Ameshinda Safari Rally mara mbili; mwaka 2022 na 2024. Ogier aliibuka mfalme wa Safari Rally mwaka 2021 na 2023.
Madereva wa Hyundai wakiongozwa na Neuville bado hawajaonja ushindi kwenye Safari Rally.
Bingwa mara mbili wa Afrika, Karan Patel na mwelekezi wake Tauseef Khan, wataongoza orodha ya madereva 15 kutoka Kenya. Karan anayedhaminiwa na benki ya KCB atapaisha Skoda Fabia R5.

Madereva wengine kutoka Kenya ni Carl Tundo/Tim Jessop (Ford Fiesta R2), Jeremiah Wahome/Victor Okundi (Skoda Fabia R5), Hamza Anwar/Adnan Din (Ford Fiesta R2), Samman Vohra/Drew Sturrock (Skoda Fabia Evo), Aakif Virani/Zahir Shah (Skoda Fabia R2), Nikhil Sachania/Deep Patel (Ford Fiesta R3) na Jasmeet Chana/Ravi Chana (Ford Fiesta R2).
Pia kunao Wakenya Rio Smith/Riyaz Ismail (Ford Fiesta R3), Minesh Rathod/Gordon Noble (Mitsubishi Lancer Evo X), Sameer Nanji/Suraj Pala (Subaru Impreza WRX), Issa Amwari/Dennis Mwenda (Mitsubishi Lancer Evo X), Evans Nzioka/Absalom Aswani (Mitsubishi Lancer Evo X), Pauline Sheghu/Linet Ayuko (Mitsubishi Lancer Evo X) na Ishmael Ombati/John Kadivane (Mitsubishi Lancer Evo IX).
Wahome,26, anarejea ulingoni baada ya kuwa nje zaidi ya mwaka. Mbio zake za mwisho zilikuwa za kitaifa za Guru Nanak Rally mwezi Novemba 2023.
Makala haya ya 72 ya Safari Rally yatajumuisha umbali wa kilomita 1,403.63 zikiwemo 384.86 za kuwania alama.