Riadha: Nuksi Februari Wakenya 7 wakikosa maadili na kupigwa marufuku
MWEZI Februari ulishuhudia Kenya ikikosa kupumua kutokana na jinamizi la ukiukaji wa maadili ya riadha kupitia matumizi ya dawa za kusisimua misuli, maarufu pufya, linalochafulia sifa miamba hao wa riadha ulimwenguni.
Geoffrey Yegon alisimamishwa kushiriki mashindano Februari 11 baada ya Kitengo cha Maadili cha Riadha (AIU) kumpata kuwa mtumiaji wa dawa iliyopigwa marufuku ya Triamcinolone. Yegon alishinda Sh5.8 milioni kunyakua taji la Standard Chartered Singapore Marathon mnamo Desemba 1, 2024.
Sheila Jepkosgei Chesang alipigwa marufuku Februari 14 kwa miaka miwili. Matumizi ya dawa haramu ya Methylprednisolone yalifanya apoteze matokeo yake yote aliyopata Oktoba 6, 2024 na baada ya Oktoba 6. Chesang alipimwa baada ya kukamata nambari mbili wakati wa Kuala Lumpur Marathon ambako alijizolea zawadi ya Sh971,250.

Ronald Kimeli Kurgat yuko nje ya mashindano tangu Februari 21 akisubiri uchunguzi dhidi yake kwa matumizi ya dawa ya Triamcinolone acetonide. Kurgat, ambaye alijishindia tuzo ya Sh2 milioni kwa kuibuka nambari moja Standard Chartered Nairobi Marathon 2024, alishiriki mbio za Hainan Danzhou Marathon nchini Uchina mwezi Desemba 2024 ambapo alikamata nafasi ya tatu.
Mshindi wa Frankfurt Marathon 2023, Sydney Marathon na Taipei Marathon 2024 Brimin Misoi Kipkorir anasubiri adhabu ya AIU. Bingwa huyo wa Nairobi City Marathon 2022 alipimwa baada ya Taipei Marathon mwezi Desemba 2024 na kupatikana na dawa haramu za EPO na Furosemide mwilini mwake.
Hasara
Careen Cheptoek ameanza kutumikia marufuku ya miaka miwili kutoka Februari 19, 2024 baada ya kupatikana ametumia dawa haramu ya Methylpresdnisolone. Cheptoek, ambaye alikamata nafasi ya pili Jakarta Marathon na Taipei Marathon mwaka jana, amepoteza matokeo yote alipata Desemba 15, 2024 na baadaye.
Nyota Edward Zakayo na Edinah Jebitok nao wanakodolea macho kupigwa marufuku baada ya Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya nchini Kenya (ADAK) kuwamulika kwa kutotoa habari za walikokuwa Februari 27.
Kwa jumla, zaidi ya Wakenya 100 wanatumikia marufuku kwa kukiuka sheria za mashindano zinazokataza matumizi ya dawa za kusisimua.