Dimba

Wawaniaji wa tuzo ya SOYA wanawake ni wanariadha pekee, hakuna Okutoyi

Na GEOFFREY ANENE April 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VITA vya kuibuka mwanamichezo bora mwanamke kwenye tuzo za kifahari za SOYA mwaka 2024 vitahusu wanariadha pekee yake – Faith Cherotich, Hellen Obiri, Beatrice Chebet, Faith Kipyegon na Ruth Chepngetich.

Orodha ya wawaniaji hao ilitangazwa Jumatano. Mshindi wa tuzo hiyo iliyoanzishwa na jagina Paul Tergat mwaka wa 2004 atajulikana wiki ijayo Aprili 16 katika jumba la mikutano la KICC mjini Nairobi.

Cherotich, 20, alishindia Kenya medali ya shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa, mnamo Agosti 6, 2024. Alifika pia fainali ya riadha za Diamond League na kuibuka mshindi Septemba 14, 2024.

Obiri, 35, alinyakua nishani ya shaba katika mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki za Paris. Alishinda Boston Marathon mwezi Aprili na kuwa nambari mbili katika New York City Marathon nchini Amerika mwaka jana.

Chebet, 25, yuko katika orodha ya wawaniaji wanaopigiwa upatu kushinda kitengo hicho cha mwanamichezo bora mwanamke ya SOYA.

Beatrice Chebet (kulia) asherehekea na Faith Kipyegon kushinda fainali ya 5,000m Michezo ya Olimpiki nchini Ufaransa mnamo Agosti 05, 2024. PICHA | JOAN PERERUAN

Alikuwa na mwaka 2024 wa kufana ambapo aliibuka bingwa wa dunia wa mbio za nyika nchini Serbia mwezi Machi; aliweka rekodi ya dunia katika mbio za mita 10,000 wakati wa Eugene Diamond League mwezi Mei akikamilisha umbali huo kwa dakika 28:54.14, na pia kuwa mwanamke wa kwanza kutimka umbali huo chini ya dakika 29.

Kwenye Olimpiki 2024, Chebet alifagia mataji ya 5,000m na 10,000m kabla kufunga Diamond League kwa kutawala 5,000m. Chebet alifunga mwaka na rekodi ya dunia ya mbio za kilomita tano barabarani baada ya kutawala Cursa dels Nassos mjini Barcelona, Uhispania kwa dakika 13:54.

Kipyegon, 31, alishinda duru ya Paris Diamond League kwa rekodi ya dunia ya 3:49.04 katika mbio za 1,500 kabla kunyakua nishani ya fedha ya 5,000m na dhahabu ya 1,500m kwenye Olimpiki mjini Paris.

Chepngetich aliandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kukamilisha 42km chini ya saa mbili na dakika 10 baada ya kushinda Chicago Marathon nchini Amerika kwa 2:09:56 mnamo Oktoba 13, 2024.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alifuta rekodi ya Kenya ya 2:14:04 yake Brigid Kosgei iliyowekwa mjini Chicago mwaka 2019, rekodi ya Chicago Marathon ya 2:13:44 iliyomilikiwa na Mholanzi Sifan Hassan mwaka 2023 na rekodi ya Afrika na dunia ya 2:11:53 iliyowekwa na Muethiopia Tigst Assefa mjini Berlin, Ujerumani mwaka 2023.

Muda bora wa Chepngetich katika 42km ulikuwa 2:14:18 akishinda Chicago Marathon mwaka 2022 kabla ya kuuimarisha kwa zaidi ya dakika tatu.

Angella Okutoyi akishiriki mashindano ya W35 International Tennis Federation (ITF) World Tour, katika uga wa Nairobi Club mnamo Januari 8, 2025. PICHA | CHRIS OMOLLO

Mwanatenisi Angella Okutoyi, ambaye alishindia Kenya dhahabu ya mchezaji mmoja kila upande kwenye Michezo ya Afrika nchini Ghana mwezi Machi 2024, hajajumuishwa.

Okutoyi, 21, ni Mkenya wa kwanza kabisa kushinda dhahabu katika michezo hiyo tangu mwaka 1978. Alinyakua pia fedha ya wachezaji wawili kila upande akishirikiana na Cynthia Wanjala.