Wikendi ya vigogo kulilia chooni, rekodi ya Liverpool ikivunjwa
LONDON, UINGEREZA
ILIKUWA wikendi ya vigogo kulilia chooni baada ya kuvurugwa kwenye ligi kubwa barani Ulaya, wikendi ambayo pia mashabiki walishuhudia rekodi nzuri ya Liverpool kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ikivunjwa na Crystal Palace ugani Selhurst Park.
Mbali na matokeo hayo, Chelsea, Manchester United na Nottingham Forest zilishindwa katika mechi zao, licha ya kuwekewa matumaini makubwa.
Kwenye mechi za EPL zilizochezwa Jumamosi, ni Manchester City pekee walioibuka na ushindi baada ya kuchapa Burnley 5-1 kwenye mechi iliyochezewa Etihad Stadium.
Kabla ya kichapo cha wikendi, Liverpool walikuwa wameshinda mechi zote tano tangu msimu huu wa 2025/2026 uanze, huku wakijivunia jumla ya pointi 15.
Baada ya Ismaila Sarr kutangulia kufungia Palace bao la kwanza mapema dakika ya tisa, Eddie Nketiah aliongeza la ushindi dakika ya 97 na kuiwezesha Palace kupanda hadi nafasi ya pili jedwalini na pointi 12 nyuma ya Liverpool ambao walipata bao la kupitia kwa Federico Chiesa.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Alexander Isak kuanza mechi kubwa katika kikosi kikuu, mechi ambayo Florian Wirtz aliingia katika nafasi ya Cody Gakpo.
Nahodha Marc Guehi aliyeibuka Mchezaji Bora wa mechi hiyo alivuruga vilivyo juhudi za washambuliaji wa Liverpool akiwemo Mohamed Salah kupenya ngome.
Akizungmza kuhusu mechi hiyo, kocha Arne Slot wa Liverpool alisema watajilaumu wenyewe kufuatia bao la pili, akidai mchezaji mmoja alizembea wakati muda ulikuwa umemalizika.
“Itabidi tujirekebishe kutokana na makosa kama haya. Walicheza vizuri na walistahili kupata ushindi huo. Tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga mabao lakini tukazipoteza. Walisoma mbinu zetu na kuvuruga mipango yetu ya kupenya. Walitusumbua sana hasa katika kipindi cha kwanza.”
Kwa upande mwingine, kocha Oliver Glasner alikipongeza kikosi chake.
“Kila mtu alijitahidi kwa sababu tulikuwa tukicheza na mabingwa watetezi. Kipindi cha pili kilikuwa kigumu, tuna bahati kupata ushindi dakika ya mwisho. Mchango wa Guehi ulitusaidia pakubwa. Tulimtarajia kung’ara kama nahodha. Ni mapema, lakini tunafurahia ushindi huu dhidi ya timu kubwa. Ni furaha kushinda mabingwa.”
Ligi hii ya EPL itaendelea kwa mechi moja ambapo Everton watakuwa nyumbani kukaribisha West Ham United katika uwanja wa Hill Dickinson kuanzia saa nne usiku.
Tottenham Hotspur 1-1 Wolves, Nottingham Forest 0-1 Sunderland, Crystal Palace 2-1 Liverpool, Chelsea 1-3 Brighton, Leeds United 2-2 Bournemouth, Manchester City 5-1 Burnley, Brentford 3-1 Manchester United.