Dimba

Young Ladies na Green Commandos FC mabingwa Kombe la Chris Oguso

Na TOTO AREGE December 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

YOUNG Ladies (mabinti) na Green Commandos FC (wanaume) ndio mabingwa wa makala ya 15 ya Kombe la Chris Oguso ambalo lilikamilika katika uwanja wa Mahanga kijijini Mungoma, Kaunti ya Vihiga.

Oguso ni mchezaji wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), kamishna wa Polisi wa Kenya na Afisa Mkuu wa Mtendaji wa mabingwa watetezi wa KPL Kenya Police FC.

Katika mashindana hayo ambayo yalidhaminiwa na kampuni ya ubashiri ya Betika, Ladies walichukua ubingwa baada ya kuwanyorosha Nice Ladies 2-1 katika fainali jana.

Ladies walicheka na wavu wa kwanza dakika ya 31 kupitia Gloria Willy.

Nao Nice Ladies wakasawazisha katika kipindi cha pili dakika ya 70 kupitia kiungo Mary Mmumbua. Kiungo Yvonne Atieno alifunga bao la ushindi dakika ya 89.

Nice na Young walifuzu fanaili baada ya ushindi wa 1-0 kila mmoja dhidi ya Wazoefu FC na Jungle FC wiki jana. Nice sasa wamepoteza fainali mara mbili baada ya kupoteza 2-1 dhidi ya Golden FC katika fainali ya mwaka jana.

“Fainali ilienda vizuri na timu zote mbili zilionyesha mchezo mzuri. Tulijiaanda vizuri na hilo limechangia ushindi wetu na hili lilitupa morale sana,” alisema Mmumbua ambaye anamiaka 15.

“Ningependa kuendelea kucheza na ninaamini nitaweza kuisaidia familia yangu. Azimio langu pia ni kuwa kocha niwafunze na wengine,” aliongezea Mumbua mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Nyakach.

Kwa upande wa wanaume, bao la kiungo Alvin Inyang’u dakika ya 14 lilitosha kuwapa Commandos ushindi wa 1-0 dhidi ya Madioli katika fainali nyingine.

Kufuzu fainali Commandos waliipepeta Green Stars 1-0 nao Madioli wakapata ushindi sawa dhidi ya Gunners FC katika nusu fainali.

Commandos walienda nyumbani na zawadi ya Sh400,000 medali na kikombe nao Madioli wakapokea Sh125,000 na medali mtawalia. Nao Young Ladies (walipata kikombe na medali) na Sh 300,000. Nice nao wahakuenda nyumbani mkono mtupu, walipata medali na kitita cha Sh 125,000 kwa kumaliza wa pili.

Timu zilizo maliza nafasi ya tatu, Gunners FC (wanaume) na Jungle FC (mabinti) walijinyakulia Sh 50,000 kila mmoja.

Walinda lango Yvonne Musungu (Young Ladies) na Julius Mugoe (Green Commandos) walituzwa kama walinda lango bora. Teresa Angesha (Wazoefu FC) na Harrison Ounza (Israel Scud) walishinda kiatu cha dhahabu kwa kufunga mabao saba kila mmoja.

Mmbua na Alvin Inyangu wa Commandos walituzwa kama wachezaji bora wa mashindano.