Makala

DINI: Kama hujafanikiwa usishushe wale waliojaliwa tayari kwa kuwadunisha

June 22nd, 2019 2 min read

Na FAUSTIN KAMUGISHA

KUSEMWA ni mtihani.

Jamii ya Wanyankole nchini Uganda ina methali isemayo, wameniteta naye huwa amewateta. Nao Wahaya husema, Unanisengenya, wanakusengenya. Wawili husengenya mmoja (Methali ya Wahaya).

Huwezi kuwazuia ndege wasiruke juu ya kichwa chako, wataruka tu, lakini wakitaka kujenga viota lazima uje juu.

Ni afadhali kuchoma mdomo kwa chakula kuliko kwa maneno.

Kusema wengine vibaya au kusemwa vibaya ni jambo baya.

“Ulimi nao ni kiungo kidogo sana lakini hujivunia mambo makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa! Ulimi pia ni kama moto” (Yakobo 3: 5-6).

“Kusema wengine vibaya ni jambo rahisi; kufikia mafanikio ni jambo gumu zaidi,” alisema Winston Churchill aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Ni rahisi kuwasema vibaya waliofanikiwa, jaribu wewe kufanikiwa kama wao, mafanikio si jambo rahisi ingawa linawezekana.

Unapowasema vibaya watoto wako ukawaita majina ya mbwa, mbuzi na nguruwe, kumbuka watu walisema wanakufanana walipozaliwa.

“Usikate kwa kisu kile unachoweza kukata kwa kijiko” (Charles Buxton).

Kama unaweza kuwakosoa watoto wako bila matusi fanya hivyo.

“Ukifanya mambo mazuri, watu watakushtaki kuwa una nia ya kujinufaisha iliyofichika, fanya mazuri vyovyote vile. Kama umefanikiwa utajipatia marafiki ambao sio wa kweli na maadui kweli, fanikiwa vyovyote vile.

Zuri utakalofanya leo litasahauliwa kesho, fanya jambo zuri vyovyote vile.

Ukweli na uwazi vinaweza kukufanya udhuriwe, kuwa mkweli na muwazi vyovyote vile. Watu wakubwa wa kike na kiume wenye mawazo makubwa wanaweza kushushwa na watu wadogo wa kiume na kike wenye mawazo madogo, fikiria makubwa vyovyote vile.

Watu huwapenda watu wanaoonewa lakini huwaiga washindi tu, pigania wanaoonewa vyovyote vile.

Unachotumiwa miaka mingi kujenga kinaweza kuharibiwa usiku mmoja, jenga kwa vyovyote vile. Ipe dunia zuri ulilonalo utakabiliwa na upinzani, ipe dunia zuri kwa vyovyote vile,” aliandika Kent M Keith.

Kama unasemwa vibaya au unawasema wengine vibaya, zingatia mambo yafuatayo. Kwanza, “Kama watu wakikusema vibaya ishi kwa namna ambayo hakuna atakayewaamini,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Plato.

Wakisema hujui lolote, jifunze mambo mbalimbali mpaka uishangaze dunia.

Pili, kama huwezi kuwa mtu mkubwa usiwashushe watu wakubwa kwa kuwasema vibaya.

Tatu, “Fikiria makosa ya wengine sehemu ya kwanza ya usiku ambapo uko macho, na makosa ya wengine sehemu ya pili ya usiku ambapo umelala” (Methali ya Kichina).

Nne, lile ambalo hulipendi katika maisha ya mwingine, risahihishe katika maisha yako.

Tano, usiseme maneno mengi ya bure. “Msema mengi humtukana mama mkwe bila kujua” (Methali ya Tanzania).”Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu” (Mithali 10:19). “Anayekosa la kusema husema kuwa mfalme amenenepa” (Methali ya Tanzania).

Kudumu daima

Sita, mazuri ya mwenzako uyaandike kwenye mwamba yadumu daima na mabaya uyaandike kwenye mchanga yapeperushwe na upepo. Saba, mazuri ya watu, fadhila za watu zitazame kwa macho mawili na makosa yao yatazame kwa jicho moja.

Nane, baya linalosemwa juu yako kama si la kweli, achana nalo. Baya linalosemwa juu yako kama si sawa usichukie. Baya linalosemwa juu yako kama ni la kweli lifanyie kazi, badilika.

Tisa, usiloweza kusema mbele ya mtu, usiseme nyuma ya mgongo wake. Umbeya ni mauaji ya kisaikolojia. Ni kama tunawaua ndugu zetu kama Kaini alivyomuua Abeli. Umbeya ni ugaidi.

“Kusemwa vibaya ni jambo ambalo tunaweza kuepuka kirahisi kwa kutosema chochote, kutofanya chochote, na kutokuwa chochote,” alisema mwanafalsafa wa Kigiriki Aristotle.

Lakini namna hiyo hatutaacha alama yoyote maishani.

Fanya zuri unaloweza kufanya licha ya kusemwa vibaya.

Unaweza kufanya jambo zuri usisikie mtu analitaja lakini tenda jambo baya utasikia likitajwa mara kwa mara kama wimbo wenye kiitikio na mashairi.

Kumbuka, mti wenye matunda ndio huwa unatupiwa mawe. Mti ambao hauna matunda hatupiwi mawe.“Kusemwa vibaya kunatuweka kwenye ushirika mmoja na Yesu lakini kuwasema wengine vibaya kunatuweka kwenye ushirika mmoja na watesaji wake,” alisema Charles H. Spurgeo.