Habari za Kaunti

Diwani apinga pendekezo la Sakaja kuruhusu wanabiashara wauze dawa katika hospitali za umma Nairobi

Na WINNIE ONYANDO September 19th, 2024 1 min read

MWENYEKITI wa Kamati ya Afya Kaunti ya Nairobi, Maurice Ochieng, amepinga pendekezo la Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na mawaziri wa kaunti la kukita maduka ya kibinafsi ya kuuza dawa karibu na hospitali za umma jijini Nairobi.

Akizungumza na Taifa Dijitali Septemba 18,2024, Bw Maurice ambaye pia ni diwani wa Mountain View alisema kuwa hatua hiyo itawakandamiza wakazi wa Nairobi.

“Namsihi waziri wa afya katika kaunti hii, Bi Suzanne Silantoi awasilishe pendekezo hilo katika bunge la kaunti,” akasema Bw Maurice.

Kando na hayo, alisema kuwa kamati mbalimbali za bunge hilo hazitaruhusu mawaziri kufanya mambo bila kuhususisha bunge.

“Umma unafaa kuhusishwa katika pendekezo kama hilo. Lazima wakazi wa Nairobi wapewe ruhusa ya kutoa maoni yao kwani wao ndio walipa ushuru,” akaongeza.

Kando na hayo, alisema kuwa kuna pendekezo la kutaka kila Hospitali ya Level 4 kuwa na afisa mtendaji, jambo ambalo anasema kuwa sharti kamati ya afya ihusishwe kabla ya kutekelezwa.

“Hatuko hapa kufanya biashara. Ikiwa mapendekezo kama hayo yatatekelezwa, basi inamaana kuwa wakazi wa Nairobi ambao ndio walipa ushuru watalazimika kulipa ushuru zaidi,” alisema.

“Wakazi wa Nairobi wanahitaji kupata matibabu kwa bei nafuu na kupata dawa kwa bei inayofaa. Hivyo sharti bunge la kaunti lihusishwe kikamilifu.”

Alilalamika kuwa mawaziri wa Kaunti ya Nairobi wana mazoea ya kutoa mapendekezo na kuyatekeleza bila kuhusisha kamati husika za bunge.