Atwanga mke mwenza kwa kudunisha mume
Na TOBBIE WEKESA
CHEBUKWABI, KIMILILI
Wenyeji wa kijiji hiki walibahatika kutazama sinema ya bure, kipusa alipomtwanga mke mwenza hadharani akimlaumu kwa kumuumbua mume wao.
Inasemekana kipusa alikerwa na tabia ya mwenzake ya kumsengenya mume wao kila aendako badala ya kumpa heshima.
Kulingana naye, mke mwenza alikuwa na mazoea ya kumchafulia sifa mzee wa boma. “Uko na ugonjwa gani wewe. Mbona usifunganye virago urudi kwenu badala ya kumharibia mzee wetu jina,” kipusa alifoka.
Punde si punde wanawake hao walianza kurushiana cheche za maneno. “Wewe ndiwe mgonjwa. Rudi ukaugulie kwako,” mke mwenza akamjibu mwenzake.
Kipusa akamuonya mwenzake aache kurandaranda akisambaza umbea wa mzee, na badala yake awe balozi mwema. “Huyu mzee sijamuona na shida yoyote. Tatizo lako ni kutoridhika. Kama unaona hafai kuwa bwanako, tafuta mwingine,” akamzomea.
Majirani walibaki kutazama tu kwa mbali huku wakistaajabishwa na matukio.
“Kama mtu ako na dosari lazima niseme. Acha kujifanya hapa,” mke mwenza alirusha jibu lake.
Kipusa hakupendezwa na madai hayo, akmkaribia mwenzake huku hasira zinampanda. “Kama umeona dosari kwake mbona utangaze huko nje. Huu mdomo wako mrefu nitaukata siku moja,” akaonya.
Mdokezi wetu asema kipusa alimrukia mke mwenza na kuanza kumuangushia makonde. “Leo huu ujinga wako utaisha. Hauwezi kumharibia jina mzee ilhali anakulisha,” kipusa akawaka huku akimpa kichapo huyo mwenzake.
Inadaiwa kidosho alijaribu kujinasua kutoka mikono ya mwenzake lakini hakutoboa.
“Umemletea mzee aibu kubwa sana. Badala ya kumsema kila wakati ni heri utafute bwana mwingine atakayekutosheleza,” kipusa alisisitiza.
Iliwalazimu majirani kuingilia kati ili kumuokoa mwanadada huyo.
“Hebu mwangalie, nguvu zenyewe hana. Kazi yake ni kutembeza migu akimsengenya mzee anayemlisha. Mshenzi sana!” kipusa akafoka.