Demu akataa kuishi na wakwe kijijini
Na JOHN MUSYOKI
MAKONGENI, THIKA
KIOJA kilishuhudiwa katika boma moja hapa kipusa alipolaumiwa na wazazi wake kwa kumtema mpenzi wake na kurejea nyumbani.
Inasemekana demu aliolewa juzi lakini hakukaa kwa muda mrefu na mume wake bila kuzozana.
Siku ya kisanga, demu alizozana na mume wake kufuatia tabia yake ya kueneza umbea mtaani, kutofanya kazi nyumbani na kuponda raha.
Jamaa alimtaka kipusa arudi mashambani kwa sababu walikuwa wakiishi mtaani lakini demu alikataa kata kata.
“Nakusihi urudi kijijini ukaishi na wazazi wangu. Kuna kazi nyingi za kufanya kuliko kulaza damu hapa chumbani. Kazi yako ni kueneza udaku tu na kuponda raha,” jamaa alimwambia mwanadada huyo.
Inasemekana mwanadada alimkemea na kumlaumu vikali kwa kumdhalilisha na kuapa kutorudi ushago.
“Eti unataka nirudi kijijini. Unataka nikafanye nini huko? Kama njama yako ni kunifukuza hapa sahau. Haukunioa niwe nakufanyia kazi. Ukinitazama hivi unadhani mimi ni mtu wa kuishi mashambani. Siendi na siendi,” demu alimwambia jamaa na akaamua kufunganya virago vyake na kurudi kwa wazazi wake.
Hata hivyo, mambo hayakumwendea vizuri wazazi wake walipomkashifu vikali.
“Umerudi hapa kufanya nini? Kwa hivyo umeachana na mume wako. Utaacha kisirani chako hadi lini? Kwa taarifa yako, kama ulidhani hapa ndipo kimbilio lako sahau. Ondoka urudi kwa mume wako. Hakuna nafasi yako wala chumba chako cha kulala hapa, nenda ukajenge ndoa yako,” babake demu alisikika akisema.
Demu alidai hangevumilia maisha ambayo mume wake alikuwa akitaka aishi.
Hata hivyo, haikujulikana iwapo wazazi wake walibadilisha nia na kukubali aishi nao.