Demu azua kisanga akitimua jombi aliyekwamilia kwake
CHANGAMWE, MOMBASA
JOMBI mmoja mtaani hapa alipata aibu ya mwaka baada ya kufurushwa na demu alipokwamilia katika nyumba yake.
Inasemekana jamaa alifutwa kazi na akahamia kwa mwanadada huyo aliyekubali kumpa hifadhi kwa kuwa walikuwa wapenzi kwa muda.
Hata hivyo, haikujulikana kilichofanya watofautiane hadi demu akaamua kumfukuza jamaa.
Kulingana na mdokezi, jamaa alikataa kuondoka alipotakiwa na demu kufunganya virago na ndipo mwanadada akakasirika na kumfukuza.
Kioja kilitokea demu aliporusha nje jamaa na kutema matusi makali.
Jamaa huyo alilazimika kuondoka plotini huku wapangaji wakimhurumia lakini kidosho hakujali kamwe japo wengi walilaani kitendo chake kwa jamaa aliyechukuliwa na wengi kuwa mumewe.
***
Apiga jirani marufuku kwake akimshuku ananyemelea mkewe
MUKUSU, MASINGA
NA JOHN MUSYOKI
JOMBI mmoja kijijini hapa alimpiga marufuku jirani kukanyaga kwake akishuku alikuwa akimnyemelea mkewe.
Siku ya kisanga, jamaa alimpata jirani huyo akipiga gumzo na mkewe kwake jioni na akamlaumu kwa kumtongoza mke wake.
“Ni kwa nini ulitembelea mke wangu bila ruhusa yangu? Nimepata fununu kuwa unanyemelea wake wa watu. Usidhani sisi ni wajinga.
Sikuamini hata kidogo kwa sababu unashukiwa kuvunja ndoa za watu. Kuanzia leo sitaki kukuona hapa kwangu. Nikikupata hapa nitakuchukulia hatua,” jamaa alimuonya jirani yake.
Mzee huyo aliingiwa na tumbojoto. Alijikunyata kama kuku aliyenyeshewa na kuondoka kuepuka hasira za mwenye boma.
***
Msupa alaumiwa kwa kuzuia kaka yake kuoa
KIPTEWIT, KERICHO
NA NICHOLAS CHERUIYOT
KIPUSA wa hapa ametakiwa akome kuwa kizuizi kwa nduguye kupata mrembo wa kuoa. Inasemekana kuwa kipusa huyo ameharibu uchumba wa nduguye mara tatu sasa.
Duru zinaarifu kuwa nduguye kidosho amekuwa akijaribu kuasi ukapera kwa muda lakini dadake huwa kizuizi bila kujulikana wazi sababu yake kufanya hivyo.
“Akipata habari kuwa nduguye amepata mchumba hutafuta mrembo huyo na kumpa fitina kuhusu kakake hadi demu anamtema kapera huyo,” mdaku akaarifu.