Demu pabaya kujilipia mahari
Na Leah Makena
MAGOGONI, THIKA
Kidosho wa hapa alikaripiwa na wazee kwa kuchukua mkopo kusaidia mumewe kulipa mahari.
Duru zasema kuwa kidosho na mpenzi wake walifika kwa wazee kuomba baraka zao ili waanze maisha kama mume na mke baada ya kuhitimu chuoni.
Kidosho alifanikiwa kupata ajira punde tu baada ya kukamilisha masomo, jambo lililomfanya babake kuwaita wazee wapinge pendekezo la binti kuolewa na jamaa ambaye hakuwa na kazi.
Mzee alisema alitaka kujengewa nyumba ya kifahari na binti yake.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kushawishi bintiye kwani alikuwa ameamua kuolewa na jamaa huyo licha ya kuwa hakuwa amefanikiwa maishani.
Kama adhabu, wazee walimtoza jamaa maelfu ya pesa kama mahari licha ya kufahamu hakuwa amefanikiwa kupata ajira. Isitoshe, walimpa kipindi cha miezi michache kulipa mahari yote na kutishia kutwaa binti yao iwapo angeshindwa kutimiza matakwa yao.
Baada ya kuwaza na kuwazua, kidosho aliamua kuchukua loni ili asaidie jamaa kulipa mahari kwa hofu ya ndoa yao kusambaratika.
Siku ya sherehe, wapenzi walifanya ‘shopping’ na kisha wakawakabidhi wazee hela walizodai jambo lililowashtua na kutaka kujua iwapo jamaa alikuwa amefanikiwa kupata kazi.
Hawakuamini walipogundua mali yote waliyopata ilikuwa bidii ya binti yao. Hapo ndipo walipomuita kando na kumzomea kwa kudekeza jamaa.
“Unawezaje kukopa loni kulipa mahari kana kwamba umekuwa mume? Si ungemuacha apambane na hali yake? Utajengea wazazi wako nyumba ya kifahari au utaendelea kulea mume? Tahadhari kwani hili dume litageuka kupe likufyonze hadi kaburini”, wazee walionya.
Waliohudhuria kikao hicho wanasema kuwa kidosho alitia masikio nta na kuendelea na maisha yake.