• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Fundi mtoro akanyaga ‘waya’ moto

Fundi mtoro akanyaga ‘waya’ moto

Na MWANDISHI WETU

DAGORETTI, Nairobi

FUNDI wa stima mtaani hapa aliyekuwa na tabia ya kunyemelea vipusa wateja wake, alijipata pabaya kwa kumchangamkia demu mgeni.

Mdokezi wetu alituarifu kuwa jamaa huyo alipenda kutangaza ufundi wake wa stima hasa kwa akina dada.

Lugha yake nzuri na ulimi wenye maneno ya kumtoa nyoka pangoni, ulivutia kinadada ambao pindi walipopata matatizo ya stima walimwita mara moja.

Siku ya tukio, polo alialikwa na dada plotini amtengenezee balbu ya chumba chake cha kulala ambayo haikuwa ikiwaka.

Alikaribishwa kwa heshima kisha akaomba stuli ya kukanyaga. Akatumia muda wake kuikagua balbu huku akimtupia mwanadada mwenye nyumba macho ya kumzuzua.

Jamaa alijifanya kushuka kidogo kwa kisingizio cha kuchukua kitu katika mkoba wake wa fundi.

Hapo ndipo alishindwa kustahimili na kupitisha mkono hadi kwenye kifua cha demu kumpapasa.

Totoshoo alishtuka, akaruka na kumpiga polo kofi kali ambalo lilimsukuma hatua kadhaa nyuma nusra kumwangusha.

“Kumbe wewe ni fisi hatari! Umewafanyia wangapi hivi? Nakuambia leo ni leo, utakiona,” demu alifoka na kumrukia akamwangusha sakafuni kutoka kwa stuli.

“Sema ulilotaka kunifanyia, la sivyo nitakuchinja kama kuku,” totoshoo alitisha.

Polo alibabaika akawa hana la kusema. Alikuwa amezoea kunyemelea vipusa bila taabu lakini siku hiyo, maji yalizidi unga.

Kelele za demu ziliwavutia wapangaji ambao walifurika chumbani mwake.

“Mnafiki huyu! Amezoea kuwatengenezea kinadada stima lakini leo amegusa ‘waya’ hatari. Nitahakikisha leo amelala seli,” mwanadada alisema akitisha kuwapigia maafisa wa polisi simu.

Haikubainika iwapo jamaa alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa kumkosea heshima demu huyo.

You can share this post!

KAMAU: Ni kosa kutowatambua mashujaa wetu nchini

Odera kuongoza wanaraga wa Kenya Simbas kufuzu kwa Kombe la...