Gen Z waanika mhubiri bandia kwa kumnunulia kamnyweso
BURETI, Kericho:
GEN Z wa eneo hili walimuaibisha jamaa aliyedai ni mhubiri mwenye uwezo wa kutenda miujiza, kwa kumwanika kuwa anapiga dozi ya vileo.
Inasemekana polo alifika eneo hili kwa kishindo na kupata umaarufu haraka kwa kuwaahidi watu kuwa wataomoka kimiujiza.
Hata hivyo,mabarobaro waliomwona jamaa huyo akijivinjari kwenye klabu za mji moja eneo hili waliamua kumuanika.
Juzi, Gen Z hao walimpata jombi akipiga dozi kwenye klabu. Jombi hakujua nia ya vijana hao na akakubali kununuliwa chupa kadhaa.
Hatimaye, mabarobaro wakampandisha jamaa huyo kwenye gari lao akiwa hajijui kisha kumpeleka hadi mtaa anakohubiri.
“Jombi aliposhukishwa aliyumbayumba asijue anaelekea wapi. Dozi ilipoisha mwilini jamaa akajua siri zake za ulaghai zilifichuka kuwa ni mhubiri feki,” mdaku akaarifu.