Dimba

FKF yazindua mkakati wa miaka minne kuinua soka ya wanawake

Na TOTO AREGE November 8th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

SHIRIKISHO la Soka Kenya (FKF) Jumatano, lilizindua mkakati wa miaka minne (2026-2029) wa Soka ya Wanawake utakao inua soka ya mabinti hao  kutoka mashinani hadi kitaifa. 

Mkakati huo uliozinduliwa katika Hoteli ya Weston, Nairobi, unajiri  wakati Harambee Starlets iliporejea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) baada ya miaka 10 na Junior Starlets ilipoweka historia kwenye Kombe la Dunia la  wachezaji wazidi miaka 17 linaloendelea nchini Morocco kwa kufuzu hatua ya 16 bora.

Mkakati huo una nguzo tano zitakazoanzia wasichana wa miaka sita hadi vituo bora vya ukuzaji vipaji (Centres of Excellence) na mikataba ya kibiashara kwa Ligi Kuu ya Wanawake (KWPL).

Kati ya 2020-2025, FKF inasema KWPL imekua hadi timu 12, Ligi Kuu ya Taifa ya Wanawake (WNSL) timu 16, Daraja la Kwanza 20, Ligi za Mikoa 88 na Ligi za Kaunti timu 289.

Zaidi ya wasichana na wanawake 10,000 sasa wanashiriki soka inayotambuliwa na FKF, huku makocha wanawake 237, waamuzi wanawake 17 na maafisa usalama 12 wakifunzwa.

FKF pia inaangazia Kampeni ya Soka ya Wanawake (WFC) iliyofikia wasichana 2,756 katika kaunti sita: Turkana (wasichana 456 kutoka shule 24), Samburu (300), Embu (300), Nairobi (900), Nakuru (400) na Busia (400).

Mgeni rasmi, Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Huduma za Watoto, Mheshimiwa Hanna Wendot Cheptumo, alisema uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuendeleza fursa kwa wasichana na wanawake kwenye michezo.

“Ninapongeza FKF na wadau wake kwa kuandaa mkakati unaotambua umuhimu wa uwekezaji, ukuzaji vipaji, mashindano bora na njia za wanawake kustawi kwenye michezo,” alisema Cheptumo.

Alitoa wito wa ushirikiano wa kudumu kati ya FKF, serikali za kitaifa na kaunti, shule, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kutafsiri mkakati huo kwa vitendo.

Rais wa FKF Hussein Mohamed anasema waraka huo si sera tu, bali ni wito wa kuchukua hatua.

“Katika FKF, tunaamini mustakabali unategemea kuwekeza katika kila sehemu ya mchezo. Hiyo inamaanisha kupanua ushiriki wa nyika, kuimarisha ukuzaji wa vijana, kuyafanya mashindano yetu kuwa ya kitaalamu, kuboresha ukocha na ulinzi, na kuunda fursa endelevu za kibiashara,” alisema Hussein.

Aliongeza: “Hii ni ahadi yetu ya kuunda mazingira ambapo kila msichana anayetamani kucheza soka anapata fursa na njia iliyo wazi ya kutimiza ndoto yake. Mafanikio hayatapimwa kwa idadi ya wasichana wanaocheza tu, bali kwa nguvu ya ligi zetu, ubora wa mashindano yetu na utendaji wa timu zetu za taifa.”

Katibu Mkuu Msaidizi wa FKF Dennis Gicheru alikiri kazi ngumu inaanza sasa.

“Mkakati huu unatoa mfumo ulio wazi wa jinsi FKF itakavyopanga na kutekeleza ukuaji. Unabadilisha maono yetu kuwa vitendo halisi na malengo yanayopimika. Sasa tunatoka kwenye kupanga na kuelekea utekelezaji,” alisema Gicheru.

Alifichua uzinduzi huo ulifanyika baada ya mafunzo ya siku nne kwa Wawakilishi 48 wa Wanawake wa Matawi ya FKF, yaliyolenga upangaji wa kimkakati, uongozi bora, ukusanyaji fedha na usimamizi bora.

“Chini ya usimamizi wa Neddy Atieno kwenye Dawati la Wanawake la FKF, sasa tunaelekea utekelezaji. Tutampa ofisi yake usaidizi wote unaohitajika ili kuhakikisha mkakati huu unatekelezwa kwa ufasaha,” aliongeza.

Mkakati unalenga wasichana 7,200 kupitia tamasha za kila mwaka kwa wasichana wa miaka 6-12 katika kaunti 12 kwa mwaka (wasichana 150 kwa kaunti) ili kufikia kaunti zote 48 ifikapo 2029. Tamasha maalum zitafanyika kaunti zilizosahaulika: Garissa, Mandera, Marsabit, Isiolo, Tana River, Lamu na Samburu.

Kwa njia ya ukuzaji vipaji, FKF itaunganisha kalenda za Kaunti, Mikoa na Taifa na kutekeleza leseni za lazima kwa vilabu vya KWPL kuanzia 2026 na WNSL 2027. Vituo viwili vya Taifa vya Umahiri vitajengwa ifikapo 2027.

Kwa uwezo, FKF itaendesha kozi tatu za ukocha kila mwaka, CAF D kwa walimu 290 kila mwaka, waamuzi wanawake 30 wapya kila mwaka na skauti wawili kwa kaunti. Pia kutakuwa na programu ya ushauri kwa wachezaji wa zamani na ufadhili wa masomo kuanzia 2027.