Dondoo

Jombi akopa godoro baada demu kulalamikia kuumwa na mbavu

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NAROK MJINI

Na NICHOLAS CHERUIYOT

ILIMBIDI Polo wa hapa kukopa godoro demu wake alipomtembelea kisha kuteta kuwa godoro lake limezeeka sana.

Inasemekana Kalameni alifurahi kipusa alipokubali kumtembelea baada ya kumpatia ahadi nyingi bila kitimiza hapo awali.

Baada ya kuwasili kipusa aliweka wazi kuwa hatalala kwa Polo iwapo godoro la kutumika ni hilo lililochakaa.

“Kipusa alipotaka kujituliza kwa kitanda aliudhika mbao za kitanda zilipomwumiza kwani gogoro la Jombi limetumika kwa miaka kadhaa,” mdaku akaarifu.

Polo akajaribu kukopa pesa kutoka wenzake plotini lakini alipokosa kufaulu alienda kwa duka la hapa na kulia asaidiwe godoro kwa mkopo.

Mwenye duka alimkopesha kisha kumwonya asiponde raha na kipusa hadi akasahau kulipa deni.

***

Kioja makalameni kupigania mke wa ndugu yao kabla hata azikwe

KATHONZWENI, MAKUENI

Na TOBBIE WEKESA

MAKALEMENI wawili ambao ni ndugu waliwaacha waombolezaji vinywa wazi walipoamua kumrushia mjane mstari hata kabla ya mumewe kuzikwa.

“Mimi ni ndugu wa marehemu mkubwa. Amenileta kwake mara nyingi. Sitashindwa sasa kujileta mwenyewe,” Polo mmoja alisema.

Vicheko vya chini kwa chini vilisikika. Jamaa wa pili wa marehemu aliitwa.

“Kunguni wa nyumba ya ndugu yangu nawajua na wananijua vizuri sana. Shemeji wewe hutaendelea kuwa mjane. Boma liko imara,” jamaa alieleza.

Inasemekana pasta aliwakemea makalameni kwa kujipigia debe wazi kabla ya marehemu kuzikwa.

***

Jombi akaripia dadake kwa kumtema mpenzi wake ambaye ni rafiki

SOY, ELDORET

Na TOBBIE WEKESA

KALAMENI mkazi wa hapa alimkemea dada yake vibaya kwa kuachana na mpenzi wake.

Inadaiwa polo hakufurahishwa na hatua aliyochukua dadake kwani jamaa aliayemuacha alikuwa rafiki yake mkubwa.

“Wewe sidhani kama utawahi pata mchumba mwingine kama huyo jamaa. Umepoteza. Siku moja utajutia,” polo alimfokea dadake.

Kipusa alidai kwamba alishafanya uamuzi na hatarudiana na jamaa.

“Acha ujinga. Hujui ulichofanya. Huyo jamaa ni rafiki yangu. Nimefaidi pakubwa kutoka kwake. Uamuzi wako ni wa kitoto,” polo alizidi kufoka.