Dondoo

Kejeli za abiria zawaachia aibu ya mwaka kondakta akitabasamu!

Na SAMUEL MUIGAI March 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ILIBIDI abiria katika matatu moja ya kuelekea Kenol, Murang’a, wanyamaze kwa aibu baada ya cheche za kumkejeli kodakta kugonga mwamba.

Safari ilianza vyema kutoka jijini na wakiwa njiani kodakta akaitisha kila mmoja nauli nao wakampokeza.

Alipomaliza kuokota senti mhudumu huyo aligundua hitilafu katika hesabu yake akaamua kuuliza abiria wahakikishe chenji aliyowapa ilikuwa sahihi na kama sivyo arekebishe.

Badala ya abiria kuhakikisha chenji ilikuwa sahihi, wakaanza kumkejeli.

“Ungetilia maanani darasa la hesabu hungekuwa unafanya makosa madogo kama haya,” mmoja wa abiria alidakia.

“Hata hakai mwenye alienda shule. Iwapo alienda angepata kazi ya maana,” akaongeza mwingine.

Baada ya kusikiza kejeli zao kwa muda kondakta akaomba kuzungumza.

“Poleni. Mnavyodhani sivyo, sijaingia shoti. Niko na pesa nyingi za hii trip kuliko inavyopaswa. Nimewapa nafasi mhakikishe kutoka upande wenu kama chenji ziko sawa, na kwa vile hakuna aliyedai chochote basi imekuwa bahati yangu,” alisema mhudumu huyo na kuketi huku akitabasamu.

Abiria hao waliingiwa na aibu. Hakuna mwenye angedai senti zozote kwani angeonekana mkora. Wote walinyamaza na kujikuna vichwa hadi mwisho wa safari.