Kisanga polo akirejeshea rafikiye mbuzi aliozawidiwa siku ya arusi
KAEWA, MASINGA
KALAMENI wa hapa alizua kisanga alipomrudishia rafiki yake mbuzi aliompatia kama zawadi siku ya harusi yake.
Hii ni baada ya rafiki ya polo kudai kwamba ndiye aliyempiga jeki kufanikisha harusi yake.
“Kama nisingempiga jeki huyu jamaa anayeringa na mkewe, walahi angebakia kuwa kapera. Mbuzi alio nao ni mimi nilimpatia kama zawadi,” jamaa alijigamba.
Inasemekana jamaa alipofikiwa na habari hizo, alimrudishia rafiki yake mbuzi wote aliompatia kama zawadi.
“Nimekurudishia mbuzi wako. Chukua ndio hao. Nataka unikome kabisa. Umeniharibia jina kila mahali. Nilidhani wewe ni rafiki yangu kumbe wewe ni mnafiki mkubwa sana. Potelea mbali,” jamaa alilalamika.
“Unanidhalilisha kila mahalii. Najuta kukuamini kama rafiki. Kuanzia leo, urafiki wangu na wewe umefikia kikomo,” jamaa aliongeza.
Tukio hilo lilishangaza majirani. Watu walimsuta jamaa kwa kumsengenya mwenzake kwa watu.