Kisura aponea kipigo kuuza mbuzi ya mume aponde raha
Na JOHN MUSYOKI
MAIUNI, MATUU
MWANADADA mmoja kutoka hapa alijipata pabaya majirani walipomkemea kwa kuuza mbuzi wa mume wake na kwenda kuponda raha na wanaume mtaani.
Duru zinasema mume wa demu huyo anafanya kazi jijini na ilikuwa nadra sana kumtembelea mkewe nyumbani kwa sababu ya kazi.
Licha ya jamaa kumtumia mke wake pesa za matumizi kila mwezi, mwanadada alikuwa na tamaa ya pesa kwa sababu ya kupenda anasa kupindukia.
Inasemekana mwanadada huyo aliuza mbuzi watano wa mumewe na akatumia pesa hizo kufurahisha wanaume mitaani.
Siku ya kioja, majirani walighadhabishwa na tabia ya mwanadada huyo na wakaamua kumfunza adabu kwa kuharibu mali ya mume wake.? Majirani walikita kambi kwake walipopata habari kuwa alipanga kuuza mbuzi wengine.
“Hei, hatutakuruhusu uendelee kuharibu mali ya mume wako. Tumekuwa tukifuatilia tabia yako. Mume wako huwa anakutumia pesa za matumizi lakini hutosheki. Unapaswa kuchunga mali ya mume wako sio kuharibu tu,” jirani mmoja alisikika akimwambia mwanadada huyo.? Penyenye zasema mwanadada alijitia ujasiri na kuwaambia majirani kuwa hawafai kuingilia masuala ya boma lake.
“Tokeni hapa kwangu ama niwachukulie hatua. Hii ni mali yangu na mume wangu. Ni haki yangu kufanya nitakalo,” aliwakemea majirani.
“Mwanamke wewe, fyata ulimi wako kabisa. Unapaswa kuheshimu wakubwa wako. Huwa unaburudisha wanaume mtaani ukiwa na pesa unapouza mbuzi wa mume wako. Tutamwambia mume wako kila kitu,” jirani mwingine alisikika akiongeza.
Hali ilipamba moto hadi majirani wakatisha kumfurusha mwanadada huyo kwa kuharibu mali ya mume wake.
Inasemekana mumewe hakuwa akipatikana kwa simu wakati wa kioja hicho.
Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya tukio hilo.
Aghalabu ndoa au mahusiano ya mbali huweza kuzaa vitimbi vya kila aina huku ndoa nyingi zikivunjika kutokana na kukosekana kwa uaminifu baina ya wapendanao.