Makahaba wamfanyia masihara kalameni
Na MAUREEN ONGALA
MAJIVUNI, KILIFI
KIZAAZAA kilitokea hapa saa saba mchana baada ya kalameni kuvamiwa na kundi la vipusa na kuvuliwa nguo.
Kulingana na mdokezi, jamaa alifika maskani ya vipusa hao wanaojishughulisha na ukahaba mtaani, mwendo wa saa nane usiku na kuagiza huduma za mmoja wao.
Yasemekana kuwa aliahidi kumlipa kidosho Sh2000 baada ya kuhudumiwa.
Ugomvi ulizuka asubuhi kalameni huyo alipodinda kutoa malipo kwa madai kwamba hakuhudumiwa, eti alikuwa mlevi chakari walipofika chumbani na hivyo alilala fofofo hadi asubuhi.
Kidosho alisisitiza kuwa alipaswa kulipwa kwa kupotezewa muda wake, wala hafai kulaumiwa kwa sababu ya kosa la mteja.
Vita vya maneno vilizuka, jamaa akashambuliwa kwa matusi na vipusa hao waliokuwa wenye hasira si haba. Lakini naye alipaza sauti akisisitiza hakuwa amepata huduma anazodaiwa malipo.
“Siogopi na sitawaogopa. Fanyeni lolote mnalotaka,” jamaa aliruka. Ilibainika kuwa awali kalameni huyo alimnunulia kidosho chake pombe katika eneo moja la burudani mjini kilifi kabla wao kufululiza chumbani kwenda kufanya mambo yao.
Mwanadada alisimulia jinsi alivyotumia Sh100 kulipa nauli ya bodaboda, pesa ambazo jamaa hakuwa amemrudishia. Vipusa wenzake waliungana naye kumvamia jamaa wakamvua nguo zote akabakia uchi wa mnyama, ili kumfunza adabu kwa kucheza na kazi yao.
Majivuni ni moja ya maeneo yanayofahamika mjini Kilifi ambako akina dada hukita kambi kufanya ukahaba.
Kulingana na mdokezi, bei yao ya chini ya hadi Sh50 ni sababu kuu ambayo imekuwa ikivutia wanaume wengi hapo ikiwemo wazee walio katika ndoa. Bei hiyo ya chini imeifanya eneo la Majivuni kubandikwa jina ‘Huduma Centre’.
Maskani hayo yanapatikana katika kichochoro cha Charo wa Mae kuelekea soko la Kibaoni.