Dondoo

Mama mkwe abeba chupi za jombi Krismasi

December 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Nicholas Cheruiyot

SOIN, KERICHO

KULIZUKA kizaazaa eneo hili chupi za polo mmoja ziliponyanyuliwa kimakosa na mama mkwe aliyekuwa amewatembelea nyumbani Krismasi.

Kulingana na udaku uliodunda mezani mwa Dondoo, mama alikuwa ametembelea familia ya binti yake na kukaa huko kwa siku kadhaa.

“Alipokewa kwa mikono miwili na kutulia nyumbani. Mwanzoni, alitaka kukaa siku moja tu, lakini mapokezi murwa aliyopewa na wenyeji wake yalimfanya aongeze siku za mapumziko huko,” mdaku alisimulia.

Inaelezwa kuwa mgeni alichinjiwa mbuzi na kupikiwa mapochopocho mengine. Akafurahia nyama pamoja na supu ya kichwa cha mbuzi iliyokuwa imechemshwa.

Kisha akatangaza kwamba muda wa kurudi ulikuwa umewadia.

Asubuhi ya siku ya kuondoka, binti yake alichukua begi ambayo ilikuwa imetumiwa na mumewe majuzi kwa safari fulani.

Akamwekea mamake nguo za maridadi alizokuwa amemnunulia kama zawadi ya Krismasi.

“Mama alifurahi sana na kupokea mfuko huo kwa shukrani tele. Akaitiwa boda boda na kuondoka baada ya kuwabariki wana hao na pia kuaga wenyeji,” mdokezi alieleza.

Safari ikawa salama salimini. Mama alipofika nyumbani kwake alikuwa na hamu ya kukagua nguo zake mpya, avae ili ang’are na kutembea kwa maringo kijijini kuonyesha zawadi alizotoka nazo kwa bintiye.

Hata hivyo, alipokuwa akitoa mavazi kwa begi hiyo mama alishangaa kuona chupi kadhaa za kiume zenye rangi tofauti humo ndani.

“Mara moja alijua ni za mume wa bintiye. Akapandwa na mori kwani lilikuwa jambo la aibu sana,” mdaku wetu aliarifu.

Moja kwa moja alimpigia simu msichana wake na kumsuta kwa kukosa kuwa mwangalifu kiasi cha kumpa begi ya suruali za mumewe.

Inasemekana mpango ulifanywa upesi na chupi zikarudishwa kwa mwenyewe siku hiyo.