Dondoo

Pasta asusia mazishi ya sonko mkono ngamu

February 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Leah Makena

KAGEENE, MAUA

Kizungumkuti kilizuka kwenye boma moja katika kijiji hiki pasta alipodinda kufika kwenye mazishi akidai mwendazake alikataa kusaidia kanisa alipokuwa hai.

Ilikuwa desturi ya pasta kufika kwa boma za washiriki wake hasa wakikumbwa na misiba ili kuwapa pole na kisha kuwasaidia kuwapa mkono wa buriani wapendwa wao.

Yasemekana bwanyenye mmoja wa hapa alikufa baada ya kuugua kwa muda mfupi na familia yake ikamuarifu pasta siku ya mazishi ili afike kuongoza ibada. Kila kitu kilikuwa shwari hadi mwendo wa saa saba pasta alipokosa kufika na familia ikawa na wasiwasi kwa sababu hakuwa ametuma ujumbe wowote kueleza kuwa angechelewa.

Pasta alitegua kitendawili alipopigiwa simu kwa kukiri kuwa hangeongoza mazishi akidai marehemu alikuwa mjeuri akiwa hai. “Sina jema la kusema kuhusu mwendazake kwani alikuwa mtu wa fitina kanisani.

Kila nilipowataka washiriki kutoa pesa kwa ajili ya injili aliwachochea akisema nilitaka kujilimbikizia mali kwa kutumia pesa zao. Isitoshe, alikataa kutoa zaka na kuapa kutohudhuria harambee yoyote kwani kwa kufanya hivyo aliona angekuwa akinilisha. Nani ataongoza mazishi ya mtu kama huyu?” pasta alijitetea.

Licha ya wazee kumuomba msamaha kwa niaba ya mwendazake, pasta alishikilia kuwa hangefika na kuwataka kutafuta mwingine kuwasaidia.

Baada ya kukosa kumshawishi, wazee walijadiliana na kumkabidhi moja wao mamlaka ya kuongoza mazishi mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Msimamo wa pasta uliwashangaza wengi na baadhi wakasema ni funzo kwa wafuasi kuchunga mienendo yao kwani wanajua fika kuwa watapata aibu iwapo watamhitaji ilhali walikuwa wakimdharau.