Dondoo

Patashika yazuka katika mazishi ya mzee

October 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN MUSYOKI

THAANA, MASINGA

KULIZUKA sokomoko katika mazishi ya mzee wa hapa watu wa ukoo walipoikemea vikali familia ya marehemu wakidai kutengwa katika shughuli nzima ya mazishi.

Watu hao wa ukoo walishangaa vipi wageni ndio walipewa jukumu la kumzika mzee.

Mwishowe, mvutano huo ulifanya ukoo wa marehemu kususia mazishi ukisema kuwa yaliandaliwa kinyume na desturi zao, tena na watu ambao hawakuwa na uhusiano na mwendazake. Majirani pia waliamua kutofika mazishini wakidai kwamba wao pia hawakuhusishwa kuyapanga wala kuhudhuria matanga katika boma la mzee huyo.

Duru zinasema siku ya mazishi boma la marehemu lilikuwa limepambwa likapambika. Hata hivyo, mambo yalikuwa yakitokota chini chini huku majirani wakishangaa kuona wageni wa nje ndio walikuwa wamealikwa kwa wingi na kupewa uhuru wa kuendesha mambo hapo.

Majirani walisema kuwa, kwa kawaida ni watu wa ukoo na majirani wanaosaidia kupika na kutekeleza majukumu mengine wakati wa maandalizi na siku ya mazishi.

Lakini walipofika kwa marehemu walionekana kutengwa na wageni hao, ambao walikuwa wamepewa hema la kujikinga na mvua ilhali wenyeji wameachwa kustahimili rasharasha hizo.

Ni dharau hilo lilifanya baadhi ya majirani kuanza kulalamika na kisha kuwachochea wenzao, ambao hatimaye waliamua kushika njia kwenda zao hata kabla ya mazishi kuanza.

“Kumbe watu wa familia ya marehemu walikuwa wamewaalika wageni na kutuona kama watu wasiofaa. Tumenyeshewa wao wakiwa ndani ya hema! Walikuwa wamepika vyakula vingi tu lakini wakawa wachoyo kwetu. Wacha wamzike marehemu sisi hatutawasumbua kama ndivyo walikuwa wamepanga,” jirani mmoja alisikika akisema.

Inasemekana baada ya mazishi wageni walikunja mahema yao na kurudi walikotoka. Haikubainika iwapo familia ilikuwa ikifuata agizo la marehemu au la, kutowahusisha majirani katika mazishi ya mpendwa wao.