Dondoo

Polo afumaniwa kwa jirani akiwa uchi

July 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CORNELIUS MUTISYA

KITENG’EI, MACHAKOS

Kizaazaa kilizuka hapa kalameni mmoja alipovamiwa na wakazi waliomfumania katika boma la jirani yake akiwa uchi.

Penyenye za mtaa zaarifu kwamba jamaa aliyeshukiwa kuwa mchawi aliokolewa na wanachama Nyumba Kumi kabla ya wakazi waliojawa na ghadhabu kumuadhibu.

Siku ya kisanga, familia moja ilisikia sauti nje ya nyumba yao mwendo wa saa sita usiku na mbwa wakaanza kubweka.

Mwenye boma alipochungulia dirishani, alipigwa na butwaa alipomuona jirani yake akiwa uchi wa mnyama na akapiga nduru.

Inasemekana kwamba wakazi walifika kwa wingi na kumpata polo nje ya mlango wa nyumba ya jirani huku akiwa na tunguri za uchawi.

Kulingana na penyenye, jamaa alipokezwa kichapo cha haja kisha akaomba msamaha akisema alikuwa ‘ajenti’ wa mama mmoja mshirikina eneo hilo.

Jamaa huyo alidai alikuwa akitumwa na mama huyo kufanya vituko vya uchawi kuua watu.

Penyenye zadai kwamba jamaa alitaja majina ya watu ambao walilenga kuua kupitia uchawi wao.

“Wakazi walibaki vinywa wazi kusikia kwamba jamaa waliyemwamini alikuwa ameamua kuwaangamiza kupitia uchawi,” mdokezi alisimulia.

Twaarifiwa kwamba, umati ulijawa na hasira za mkizi na ukatisha kumteketeza ili awe funzo kwa wachawi wengine.

Hata hivyo, aliokolewa na wanachama wa Nyumba Kumi waliosema madai yake hayangeweza kuaminika bila uchunguzi.

Inasemekana kuwa hasira za wakazi zilichochewa na pasta mmoja aliyetabiri kuwa watu wanaotumia nguvu za giza wameongezeka eneo hili.

“Uchawi umekithiri eneo hili. Hatutakaa kitako huku watu wetu wakiaga dunia ovyo ovyo kupitia ibada za giza. Wachawi na wanaoabudu nguvu za giza ni lazima wakomeshwe kwa maombi ili Mungu atamalaki kati yetu,” pasta huyo alinukuliwa akisema.