Polo alazimishwa kulea mtoto wa nje ili adumishe ndoa
Na Ludovick Mbogholi
JUNDA, KISAUNI
POLO wa hapa alijipata katika njia panda baada ya kipusa aliyemuoa kumlazimisha achukue mtoto aliyezaa nje ya ndoa na kumlea.
Inasemekana mwanadada alimlazimisha jamaa kumchukua mtoto huyo amlee kama hakikisho kwamba hatamuacha akijifungua.
“Mlete mwanao uliyezaa nje ya ndoa na umlee,” kipusa alimwambia polo. Jamaa alishanga kusikia takwa la mwanadada. “Kwa nini nimlete na mamake sikumuoa,” polo alijibu.
Mkewe alimweleza, “Nyinyi hamwaminiki, mnapachika mimba wanawake na kuwaachia mzigo wa ulezi, mnahepa majukumu,” alidai kipusa.
“Unanilazimisha nimlete ilhali sikumuoa mama yake,” polo alisisitiza.
“Hata kama haukumuoa, ni mwanamke kama mimi, kama wanijali onyesha uaminifu kwa mwanao. Najuaje nikizaa hutanifanyia ulivyomfanyia mwenzangu,” kipusa alimwambia. Jamaa alijaribu kumweleza mkewe kwamba hakuwa na nia ya kumuacha.
“Sikuachi hata ukinizalia, sikukuacha uliposhika mimba, nikuache utakaponizalia?” polo alimuuliza kipusa.
“Kama mwenzangu ulimtupa na kumsahau na mwanao, utashindwaje kunifanyia hayo,” kipusa alishikilia.
Polo aliduwaa akawaza na kuwazua na mwishowe akaamua kutafuta ushauri wa wazee.
“Asemayo mkeo ni kweli, vijana wa leo hawaaminiki, wakipachika wasichana mimba huwatoroka na kuwaachia mzigo. Hata huyu mkeo mkikosana unaweza kumwacha aende na jukumu kubwa la ulezi wa mwanao atakayezaliwa, muonyeshe upendo umletee mwanao,” wazee walimshauri polo.
Yasemekana kipusa alikuwa na mimba ya miezi sita na alihofia mumewe angemwacha atakapozaa. “Mimba inamsumbua, nikimleta ataanza kulalamika simjali,” polo alidai mbele ya wazee.
Kipusa alitisha kuondoka jamaa asipomleta mtoto huyo akihofia kuachwa na ilibidi jamaa akubali takwa na mkewe.
“Basi nitamleta bora unisaidie kumlea,” alisema polo na kipusa akatulia.