Dondoo

Polo na mkewe wapigishwa raundi baada ya kunaswa na mboga za wizi

February 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Cornelius Mutisya

Kaviani, Machakos

SINEMA ya bwerere ilishuhudiwa janibu hizi polo na mkewe walipozungushwa sokoni wakibebeshwa magunia yaliyojaa sukumawiki walizopatikana wakiiba katika shamba la jirani yao.

Penyenye zaarifu kuwa, wawili hawa walikuwa wauzaji maarufu wa mboga na matunda katika soko mjini Machakos.

Hakuna aliyekuwa akidhani kuwa wawili hao walikuwa wakiuza mboga na matunda ya wizi kutokana na heshima kubwa waliyokuwa nayo katika jamii,” alisema mpambe wetu.

Kulingana na mdaku wetu, jombi na mkewe walipata ufanisi usiomithilika kwa sababu biashara yao ilinoga na kushamiri mno. Hata hivyo, hakuna aliyejua walikokuwa wakitoa mboga na matunda hayo.

”Wawili hao walikuwa wakipakia sukumawiki na avokado katika magunia majira ya usiku na kuenda kuchuuza mjini Machakos” alisema mdokezi.

Inasemekana kwamba, jirani wao aliyekuwa mkulima maarufu wa sukuma wiki alipata zimevunwa na watu wasiojulikana na akapiga ripoti kwa maafisa wa nyumba kumi na uchunguzi mkali ukaanzishwa.

Kwa mastaajabu makubwa, polo na mkewe walifumaniwa shambani wakitia sukumawiki katika magunia.

Hata hivyo, maji yalizidi unga walipoulizwa aliyewapa ruhusa ya kuvuna mboga hizo na wakakosa kupeana jawabu la kuridhisha.

Walibambwa na kulazimishwa kubeba magunia hayo hadi sokoni hapa na wakaanza kuzungushwa ili waonekane na umati.

”Wawili hao walizungushwa sokoni hapa kwa muda mrefu mpaka wakachoka,” alisema mpambe wetu.

Twaarifiwa kwamba, washukiwa hao walikubali kutekeleza wizi huo na wakaamriwa walipe mwenye mboga hizo gharama yote ya kukuza na kutunza, la sivyo, wapelekwe kituo cha polisi ili wakabiliane na mkono mrefu wa sheria.

”Kalameni alimlipa mkulima huyo gharama yake yote na akaapa kutorudia kosa hilo tena” asema mdaku wetu.