Dondoo

Pombe ya bwerere ilivyosababisha jombi kuvunjika mkono

January 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

POLO mmoja katika Kaunti ya Murang’a anauguza majeraha ya kuvunjika mkono wake wa kulia, baada ya kuanguka akibugia pombe ya kununuliwa.

Inasemekana jamaa aliingia katika baa moja ya Mjini Murang’a na akapata sonko wa mtaa aliyekuwa anastarehe na marafiki zake.

“Wewe tajiri ni mchoyo sana na inaonekana Mungu alikubariki na pesa lakini hutaki kula na mahasla mtaani kama shukrani kwa Maulana. Fanya mambo ikiwa utafilisika, tutakuandalia harambee tukuchangie,” polo akafoka.

Badala ya sonko wa watu aghadhabike, kwa upole alimwambia jombi aketi apewe pombe mpaka atosheke.

“Polo aliitisha pombe aina ya makali kwa jina ‘Konyagi’. Akamaliza ya kwanza kwa mpigo hata bila kuiweka maji. Akaagiza ya pili ambayo pia alibugia. Kisha akaagiza ya tatu na ndipo kisanga cha saa tano usiku ndani ya baa hiyo kilizuka,” asema mdokezi.

Duru zinaarifu kalameni aliamka kutoka kwa kiti chake akionekana hoi, akatoa matamshi ambayo hayakueleweka huku jaribio lake la kwanza kupiga hatua ya kutembea ili aelekee nyumbani likimwangusha chini kwa kishindo na akalalia mkono wake.

“Hata bila kuambiwa tulijua amevunjika mkono wake kwa kuwa ulitoa sauti kama ya kuni kavu ikivunjwa. Ulevi aliokuwa nao hata haukumpa hisia za uchungu na alijigaragaza sakafuni akijaribu kuamka huku nao mkono ukionekana kufura kwa kasi,” akasema mdokezi wetu.

Meza ya Dondoo kwamba yule sonko ndiye tena alimchukua polo kwa gari lake na akamwasilisha hadi katika hospitali ya Murang’a, ambapo amelazwa akitarajiwa kutwikwa bili ya zaidi ya Sh100, 000 kwa tamaa ya pombe ya Sh750.

[email protected]