• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Siasa zaletea buda balaa nyumbani

Siasa zaletea buda balaa nyumbani

Na NICHOLAS CHERUIYOT

BAHATI, Nakuru

BUDA wa hapa aliingiwa na tumbojoto alipofika nyumbani na kupata kikao cha wafuasi waliofika kumshawishi mkewe awanie kiti cha kisiasa.

Inaelezwa kuwa mkewe ni msomi na mchangamfu mno, jambo ambalo limewafanya wakazi wa hapa kumtaka agombee kiti cha udiwani.

“Kwa muda kabla ya siku ya tukio, fununu ilienea kwamba mwanadada huyo atasimama kuomba kura, lakini yeye mwenyewe akawa kimya kuhusu jambo hilo. Wengine walidai alikuwa akifanya mashauriano ya kina na mumewe kabla ya kutangazia umma,” mdaku alieleza meza ya ‘Dondoo’.

Hata hivyo, hivi majuzi buda alinukuliwa mtaani akisema kuwa tangu mkewe apate elimu ya juu kumliko amevimba kichwa na kudinda kumpa nafasi ya kupumua, wacha hata ya kunguruma bomani mwake.

“Alihitimu chuo kutokana na ufadhili wangu na badala ya shukrani ameanza kunipiga mateke kama punda. Siwezi kumruhusu kuingia siasa, huo utakuwa mwisho wangu,” polo alisikika akiteta kwenye gumzo mtaani.

Siku ya tukio, jamaa alikuwa ameenda kushauriana na mwandani wake katika kijiji jirani na aliporudi aliduwaa kupata watu wakifanya mkutano kwenye kivuli nje ya nyumba yake.

“Alibaki kinywa wazi kufahamishwa kwamba mkewe anapewa baraka za kuwania kiti cha uongozi. Alikasirika kwamba alitengwa katika uamuzi huo pasipo kupewa arifa zozote,” mdokezi alisema.

Moja kwa moja alianza kuzusha, lakini akashauriwa na wageni atulize boli ili aelezwe zaidi.

Walipomweleza kuwa angefaidika mkewe akiwa mheshimiwa, alikubali japo shingo upande.

You can share this post!

Rais awasihi Wakenya waongeze imani kwa Mungu

Waajiri waonywa dhidi ya kufuta wafanyakazi

adminleo