Dondoo

Tajiri azushia pasta kunyimwa kiti kanisani

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Leah Makena

KISAYANI, KIBWEZI

Mama wa hapa alishangaza washiriki alipotwaa vitambaa alivyokuwa amepeana kanisani na kuapa kutohudhuria ibada alipokosa kuchaguliwa kama kiongozi wa akina mama.

Inasemekana kuwa mama alikuwa mshiriki wa kanisa hilo kwa miaka mingi na alikuwa akichangia pakubwa kwa sababu ana mali nyingi.

Kulingana na mdokezi, mama alijitolea kwa hali na mali kuhakikisha kuwa ujenzi wa kanisa ulikuwa ukisonga mbele. Kwa muda wote huo, alikuwa kiongozi wa akina mama kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Hivi majuzi, alishangaa alipokosa wadhifa wowote baada ya uchaguzi kufanyika na alimtaka pasta kueleza sababu ya kumtema.

Mtumishi wa Mungu alijiondolea lawama na kusema kuwa alikuwa amesafiri wakati wa uchaguzi na alitwika wazee wa kanisa jukumu hilo.

Mama hakuamini alipowataka wazee kuweka wazi kilichojiri kwani walimpa vidokezo vilivyomchoma moyo wakidai alikuwa amekalia pasta kutokana na kimbelembele na kujigamba kwake.

“Tulionelea ni vyema mama mwingine achukue wadhifa wako ili tupate mabadiliko kiasi. Tunakushukuru kwa muda uliohudumu ila sio lazima uchaguliwe miaka nenda miaka rudi. Asante kwa msaada wako ila kwa sasa tumeonelea upumzike,” wazee walimpasha.

Inasemekana kuwa mama alipandwa na mori kusikia matamshi ya wazee.

Siku ya ibada iliyofuata, alitwaa vitambaa vilivyokuwa vikitumiwa kwenye altari na kutishia kuchukua vitu vingine kadha alivyokuwa amechangia kanisani iwapo hawangempa nafasi ya kuongoza.

Hata hivyo, wazee hawakushtuliwa na matamshi yake kwani walimtaka achangamke na kutwaa alichodhani kilikuwa chake mapema wakimlaumu kwa kugeuza kanisa kuwa nyumba yake.