Dondoo

Wakabili pasta kwa kuwaita wenye dhambi

May 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na LEAH MAKENA

NAARI, MERU

Pasta wa hapa alijipata mateka alipofungiwa kwenye ofisi yake kwa saa kadhaa kwa kuondoa majina ya waumini kwenye sajili ya ushirika akidai walikuwa wenye dhambi.

Mchungaji huyo alidai kwamba baadhi ya washiriki walikuwa wameoa mabibi wengi, hulewa chakari na hata kutumia mali ya kanisa kwenye shughuli zao bila kujali.

Inasemekana kuwa kila walipoenda kinyume na mafunzo ya Kikristo na sheria za kanisa, washiriki hao walikuwa wakifumba macho mapasta wa awali kwa hela ili anyamazie makosa yao wakidai kila mtu ni mwenye dhambi na hakuna aliyekuwa mkamilifu mbele ya Mungu.

Kizungumkuti kilizuka pasta alipohamishiwa kanisa hilo. Baada ya kufanya uchunguzi na kujua kuwa washiriki walikuwa wakioga dhambini, pasta aliwapa onyo lakini wakadinda kubadilisha mienendo wakidai walikuwa wamezoa maisha ya starehe.

Hapo ndipo mtumishi aliita kikao cha kamati kuu ya kanisa na kuondoa asilimia kubwa kwenye ushirika akitaja kila mmoja kulingana na dhambi zake.

Inasemekana kwenye ibada iliyofuata, washiriki walipashwa habari na wakaanza manung’uniko wakimtaja pasta kuwa mjuaji kwa kujaribu kuwatishia maisha.

Siku ya kioja, baadhi ya washiriki walivamia pasta akiwa kwa ofisi yake, wakachukua funguo na kufunga mlango.

Pasta alipogundua kuwa mambo hayakuwa shwari alianza kuvutia washiriki waya ili wafike kumnusuru. Kwa zaidi ya saa nane, pasta aling’ang’ana bila kufanikiwa kwani wengi walimzimia simu na kukataa kuzungumza naye.

Aliamua kumuita mke wake aliyefika na vijana wawili na wakalazimika kuvunja mlango.

Mgogoro kati ya pasta na washiriki uliendelea hadi akahamishwa kutoka kanisa hilo.