Habari za Kitaifa

Drama kortini mwanaharakati akiachiliwa huru

Na RICHARD MUNGUTI September 4th, 2024 1 min read

KIZAAZAA kilitokea katika mahakama ya Milimani ambapo mwanaharakati Julius Mwangi alizua kioja kwa kupinga serikali ikiomba muda imfungulie mashtaka Boniface Mwangi.

Boniface ambaye pia ni mwanaharakati tajika alipinga vikali hatua ya polisi kuitisha muda zaidi kukamilisha uchunguzi kisha kumfungulia kesi.

“Sitakubali hii mahakama itumike vibaya. Sitaruhusu serikali imfungulie mashtaka Boniface Mwangi yasiyo na mbele wala nyuma. Kuandamana ni haki ya kila mwananchi,” Julius alisema huku akitifua kivumbi.

Akishika bango lenye maandishi ya kuhoji waliko wanaharakati waliotekwa nyara pamoja na waandamanaji wa Gen Z, Julius alivuruga mahakama na kusababisha mtafaruku.

Mwanaharakati Boniface Mwangi (kushoto) alipoachiliwa na mahakama ya Milimani. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Maafisa wa polisi walimkabili Julius na kumfurusha nje ya mahakama.

Utulivu ulirejelea tena kwenye mazingira ya korti, kisha kiongozi wa mashtaka akaomba apewe muda wa wiki mbili kukamilisha uchunguzi ndipo mashtaka yawasilishwe.

Bw Boniface aliomba aachiliwe huru akisema polisi wamezembea kazini na kwamba anatakiwa kuachiliwa.

Akitoa uamuzi, hakimu alisema upande wa mashtaka haujawasilisha ushahidi dhidi ya Mwangi na kumwachilia huru pamoja na wenzake.

Mahakama ilielezwa kuwa serikali haijawasilisha ushahidi dhidi ya Mwangi.