Makala

Eti pesa ngapi? Dai wazee waliweka bei ya kumwoa Betty Maina kuwa Sh300 milioni

January 27th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

HIVI majuzi, mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a Betty Maina alilipiwa mahari na mbunge wa Mathira Eric Wamumbi, 37.

Hafla ya ulipaji mahari katika kijiji cha Kangari kilichoko eneobunge la Kigumo ndani ya Kaunti ya Murang’a ilihudhuriwa na Rais William Ruto pamoja na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Bw Gachagua ndiye alikuwa mzee wa upande wa Bw Wamumbi na alilia kwamba hajawahi kushuhudia mahari ya juu katika ndoa nyingine yoyote ambayo ameshiriki kama mzee.

“Nusura tulemewe kulipa mahari licha ya kuwa sisi wa kutoka Kaunti ya Nyeri si maskini na wala si watu mkono gamu,” akasema Bw Gachagua.

Sasa, kumejitokeza mdokezi aliyekuwa katika kikao hicho cha ulipaji mahari na anadai kwamba gharama ya Bi Maina ilikuwa Sh300 milioni!

Jinsi tu ambavyo Bw Gachagua alikuwa amefichua, wazee kutoka upande wa Bi Maina walishikilia kwamba walikuwa wakiuza ‘mali safi’ iliyokuwa imewekezewa mtaji mkuu wa faida.

“Mimi sijawahi kushuhudia mahari ya juu na yanayosukumwa kwa bidii jinsi hiyo. Nusura tulemewe. Tuliambiwa msichana wao ni mrembo, amesoma sana na amepata cheo cha kisiasa kilicho na mshahara mkubwa na hayo ndiyo manufaa tuliyokuwa tunachukua kutoka kwa wazazi wake,” Bw Gachagua akalia baada ya kumalizana na bili hiyo.

Naibu Rais alilia kwamba ng’ombe na mbuzi ambao walidaiwa kuhesabika ni mahari, walikuwa ni wengi ajabu.

“Yalikuwa ni mamilioni ya pesa na tulitoka kwa kikao hicho tukiwa tumetolewa kijasho chembamba na tukiwa tumevamiwa kwa mifuko kisawasawa,” akaungama.

Aliongeza kwamba kwa sasa hiyo sio hoja kwa kuwa “tumefanikiwa kustahimili mipigo na sasa mali ni ya Bw Wamumbi ambapo mchana Bi Maina atakuwa akiwajibikia majukumu ya uongozi Murang’a lakini jioni anaingia Nyeri kuendeleza majukumu yake ya ndoa”.

Bw Gachagua alisema kwamba gharama hiyo ya mahari ilifaa izawadiwe kwa watoto kuzaliwa ndani ya ndoa hiyo.

Sasa, mdokezi wetu anasema kwamba mahari hiyo iligawanywa kwa awamu tatu za Bi Maina ambapo malezi, masomo, na ufanisi wa hadhi vilitozwa Sh100 milioni kwa kila mojawapo.

Mdokezi alifichua kwamba kila mara Bw Gachagua na wazee wenzake waliposema wanahisi kulemewa, walikuwa wakikumbushwa kwamba wangeishia kumuaibisha Rais ambaye alikuwa nje akingojea fursa yake ya kubariki hafla hiyo.

“Ilibidi wazee hao wa Bw Gachagua kusaka usaidizi kutoka kwa wanasiasa zaidi ya 20 ambao walikuwa wamefika katika hafla hiyo ili kuafikia gharama waliyokuwa wametwikwa,” akasema mdokezi.

Bi Maina alisomea Shule ya Msingi ya Kangari Upcountry kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Naaro ambapo alifanya Mtihani wa Kitaifa wa Kudato cha Nne (KCSE) mwaka wa 2007.

Kabla ya kujiunga na siasa mwaka wa 2022, alihitimu na shahada ya Masuala ya Maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU).

Kisiasa, Bi Maina ambaye ndio anapambana kumalizana na miaka ya 30, hufahamika kama ‘Betty e sawa’ na ndiye mtunzi wa wimbo “tugokira tene tugathure Ruto (tutaamka mapema tukamchague William Ruto kuwa Rais)” mwaka wa 2022.

Kabla ya kuoana, Betty na Wamumbi walikuwa katika husiano tofauti na ambapo kila mmoja alikuwa na watoto wawili na kwa sasa, kabla waongeze hao walioelekezwa na Bw Gachagua wapate, wanalea wanne hao kwa pamoja.

 [email protected]