HabariHabari za Kitaifa

Gaidi Grant amaliza kifungo Kenya, arudishwa Uingereza kujibu mashtaka

Na BRIAN OCHARO August 10th, 2024 1 min read

GAIDI Jermaine Grant hatimaye amerejeshwa kwao nchini Uingereza baada ya kusotea jela Kenya kwa miaka 13 tangu kukamatwa kwake mnamo 2011.

Grant mwenye umri wa miaka 41 alichukuliwa kutoka Gereza la Kamiti baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka 13 kwa makosa mbalimbali likiwa ni pamoja na kupatikana na vilipuzi.

Ripoti zinaonyesha kuwa wawakilishi katika idara ya usalama nchini walimpandisha Grant ndege na kumsafirisha hadi Uingereza siku ya Alhamisi, ambapo alikamatwa mara tu alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow.

Gaidi huyo ambaye amekuwa akihusishwa na mshukiwa wa ugaidi Samantha Lewthwaite, sasa anazuiliwa London kwa Sheria ya Ugaidi.

Grant alisafirishwa kwao mwaka mmoja tu baada ya serikali kupitia Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuiomba Mahakama Kuu kumruhusu kurejeshwa nchini mwake baada ya kukamilisha kifungo.

Katika ombi lililowasilishwa kortini Julai 2023, Idara ya Mashtaka ya Umma ODPP ilimtaka Jaji Ann Ong’injo kuomba na kuchunguza rekodi ya kesi za uhalifu za mahakama  kutambua hukumu aliyopewa Grant.

ODPP ilitoa ombi hili kwani mahakama ya chini iliyosikiliza kesi yake na kumpata na hatia haikutoa amri kuhusu hatma yake baada ya kukamilisha hukumu yake kwa vile alikuwa rai wa kigeni.

Grant hakupinga ombi hili akisema hakuwa na shida yoyote hata akirejeshwa kwao Uingereza.