HabariHabari za Kaunti

Gavana Nassir asema wabunge wanalemaza ugatuzi

Na WINNIE ATIENO August 11th, 2024 2 min read

GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir amekashifu Bunge la Kitaifa akisema imeshindwa kulinda ugatuzi huku serikali za kaunti zikiendelea kucheleweshewa mgao huku zikipunguziwa fedha. 

Bw Nassir alisema ni Bunge la Seneti pekee ambalo limekuwa mstari wa mbele kulinda ugatuzi.

Gavana huyu amewakia  wabunge akisema wameshirikiana na serikali kuu kukandamiza serikali za kaunti.

Akizungumza katika mkutano wa kisiasa huko Jomvu, Bw Nassir alisema serikali za kaunti zinafaa kupokea Sh400 bilioni.

Bunge la kitaifa lilipunguza fedha hizo hadi Sh380 bilioni.

“Inasikitisha kuwa Bunge la Kitaifa lilikwenda na kukubaliana na serikali kuu ya kwamba serikali za kaunti zipunguziwe fedha za ugatuzi kutoka Sh400 bilioni hadi Sh380 bilioni. Ninashukuru maseneta ambao wametuhakikishia kwamba watalinda ugatuzi,” alisema Gavana Nassir.

Aliitaka serikali kuu kuwajibika na kuhakikisha serikali za kaunti zinapokea fedha za ugatuzi kwa mujibu wa sheria na hata katiba.

Bw Nassir alisema licha ya serikali kuu kuwa na changamoto za ukusanyaji wa ushuru au mapato, mzigo huo haufai kubebwa na serikali za kaunti.

Alisema ni wajibu wa serikali kuu kupunguza matumizi yake endapo inakabiliwa na changamoto za kifedha badala ya kupunguza za ugatuzi.

“Kwanza nalikosoa Bunge la Kitaifa, mlifanya makosa kikatiba, nashukuru bunge la seneti kwa kulinda katiba. Hivi karibuni Tume ya Mgao wa Mapato Nchini (CRA) italeta Miswada ya Fedha katika Bunge la Seneti, kuna dalili kaunti kadhaa za Pwani zitaumia,” akaongeza naibu huyo kiongozi wa chama cha ODM.

Aliwasihi maseneta wahakikishe kuna usawa na haki katika ugavi wa fedha.

Bw Nassir pia alijitetea akisema amekuwa akitumia fedha za ugatuzi kwa ajili ya maendeleo ikiwemo kuhakikisha mishahara ya wafanyikazi inalipwa kwa wakati na wanakandarasi waliojenga barabara pia wanalipwa.

“Sijawahi kurejesha fedha kwa serikali kuu, hata kama tunacheleweshewa fedha kwa muda wa miezi. Kwanza kama serikali ya kaunti tunadai fedha zaidi,” akasema.

Alisema alipunguza ada za leseni kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ili kupiga jeki biashara.

Bw Nassir alikuwa anawajibu wanasiasa na wapinzani wake wakubwa ambao walimtuhumu kuwa hawekezi kwenye sekta ya biashara kwa kuwapa vijana na kina mama mikopo.

Wiki iliyopita wanasiasa wa Mombasa wakiwemo Seneta Mohammed Faki, Spika wa Bunge la Mombasa Aharub Katri, Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi na wengineo walimkashifu Gavana Nassir.

Walisema ameshindwa kuwekeza kwenye sekta ya ajira miongoni mwa vijana kwa kuwapa mikopo ili wafanye biashara.

Wanasiasa wa Mombasa walidai kuwa kuna fedha ambazo Gavana Nassir alirejeshea serikali kuu kwa kushindwa kuzitumia kuimarisha ugatuzi.

Hata hivyo Bw Nassir aliwaambia waache kuingiza siasa kwenye suala tata la ajira akiwasihi washirikiane kuimarisha ugatuzi.

“Nitarejea hapa Jomvu kutoa fedha za vikundi kwa vijana na kina mama wafanye biashara,” alisema Bw Nassir.