Habari za Kitaifa

Gavana Nyaribo alivyopona licha ya madiwani wengi kupiga kura ya kumtimua Nyamira

Na WYCLIFFE NYABERI September 17th, 2024 1 min read

GAVANA wa Nyamira Amos Nyaribo ameponea kutimuliwa kwa tundu la sindano mswada uliolenga kumng’atua afisini katika jaribio la pili ulipotibuka.

Katika kikao cha kujadili mswada huo mnamo Jumanne, Septemba 17, 2024, madiwani 22 walipiga kura ya kumng’atua mamlakani gavana Nyaribo ilhali 12 wakapiga kura kumuokoa.

Kulingana na jinsi kura hizo zilivyopigwa, kigezo cha thuluthi mbili kinachohitajika ili kumng’atua gavana huyo hakikuafikiwa.

‘Kufuatia jinsi kura zilivyopigwa, mswada huu umekosa kutimiza kigezo cha thuluthi mbili kinachohitajika kisheria na hivyo basi umeanguka,’ Spika wa Nyamira Enoch Okero alisema

Kiongozi huyo wa chama cha United Progressive Alliance (UPA), anatuhumiwa kwa makosa mawili ambayo ni ukiukaji wa Katiba na matumizi mabaya ya afisi yake.

Mswada huo uliwasilishwa bungeni wiki jana na diwani mteule wa chama cha Wiper Evans Juma Matunda.

Hii ni mara ya pili madiwani wa Nyamira kujaribu kumng’atua afisini Bw Nyaribo. Mnamo Oktoba mwaka wa 2023, madiwani hao waliwasilisha mswada mwingine lakini ukatibuka.

Katika mswada wa awali, madiwani 18 walitaka Nyaribo aende nyumbani ilhali 16 walipiga kura ya kumwokoa.

Kwa wakati huo, Nyaribo alituhumiwa kwa makosa 12.