Korti yaidhinisha mhadhiri kufutwa kazi kwa kufanya mapenzi na mwanafunzi
MAHAKAMA ya Leba jijini Nairobi imeidhinisha kufutwa kazi kwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Murang’a kwa kuhusika katika uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi, ikisisitiza kuwa tabia kama hiyo ni ukiukaji mkubwa wa maadili ya kazi.
Mahakama ilibaini kuwa mhadhiri huyo, Bw NKB, alikuwa na uhusiano usiofaa na mwanafunzi aliyekuwa akisomea Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce), huku yeye akiwa mhadhiri katika Idara ya Uhandisi wa Umeme na Elektroniki.
Jaji Mathews Nduma aliamua kuwa tabia hiyo ilikiuka kanuni za maadili za Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Murang’a, na kufutwa kazi kwa NKB mwezi Machi 2020 kulifanywa kwa misingi halali.
Mahakama ilitupilia mbali madai ya mhadhiri huyo ya kutaka arejeshwe kazini na dai lake la fidia ya Sh22 milioni kwa hasara ya ajira, kuharibiwa kwa sifa yake na madai ya ukiukaji wa haki zake za ajira.
“Mahakama imeridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa na shahidi wa mshtakiwa wa kwanza kwa mizani ya uwezekano, unaonyesha kuwa mlalamishi alikuwa na uhusiano wa kingono na mwanafunzi katika chuo kikuu alikokuwa akifundisha.
Alimletea usumbufu, mateso ya kihisia na kiakili, hali iliyohitaji ushauri nasaha ambapo tabia hiyo isiyofaa ilifichuliwa,” alisema Jaji Nduma.
Mahakama ilieleza kuwa NKB alipitia mchakato wa kinidhamu na alipewa nafasi ya kujitetea lakini alishindwa kujinasua dhidi ya tuhuma za utovu wa nidhamu.
Mwanafunzi huyo alitoa ushahidi kuwa alijiunga na chuo hicho mwezi Agosti 2018 kupitia mpango wa kazi na masomo.
Alikutana na NKB mwezi Agosti 2019 karibu na maabara ya umeme ambapo alikuwa akifanya kazi. Alitambulishwa kwake na msimamizi wake.
Walibadilishana nambari za simu na kuanza kuzungumza. Mwanafunzi huyo alisema kuwa NKB alimrai kwa maneno matamu na kwa muda akaanza kumwamini.
Alisema kuwa alitembelea nyumba ya NKB mjini Murang’a mara tatu kati ya Agosti na Septemba na kulala huko. Asubuhi, angepewa Sh100 kama nauli ya kurudi chuoni.
Baadaye, alisema, Bw NKB alimtambulisha kwa mpenzi wake lakini akaendelea kumsumbua kwa kumfuatilia kila mara hadi ikawa vigumu kwake kustahimili.
Aliripoti suala hilo katika ofisi ya ushauri nasaha ya chuo ambapo alihudumiwa na Bi Ronoh Goretti.
Mahakama iliambiwa kuwa Bi Goretti alimshauri aripoti suala hilo kwa Naibu Chansela, baada ya hapo mwanafunzi aliandika barua rasmi kuelezea masaibu yake.
Akipinga kufutwa kazi kwake, Bw NKB alidai kuwa hakuruhusiwa kumhoji mwanafunzi huyo ili kuthibitisha ukweli wa madai yake.
Alisema kuwa mwanafunzi huyo hakuwahi kuwasilisha malalamishi rasmi wala kiapo, na hakuna ripoti yoyote ya polisi iliyowasilishwa kuhusu madai hayo.
Katika utetezi wake, alidai alikuwa tu akimsaidia mwanafunzi huyo ikiwemo kumlipia dawa na kumtumia pesa mama yake.
Alisema mchakato wa kinidhamu ulikiuka haki asili na haki za kikatiba.
Hata hivyo, Afisa Mkuu wa Usalama wa Chuo Kikuu cha Murang’a, Bw Felix Kimotho, alitoa ushahidi kuwa kesi hiyo iliripotiwa kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Murang’a, Bw NKB aliitwa mwezi Februari 2021 kuandika taarifa baada ya mwanafunzi kudai kubakwa.
Hakuna mashtaka ya jinai yaliyofunguliwa dhidi yake.
Katika uamuzi wake, mahakama ilibaini kuwa kufutwa kazi kwa Bw NKB kulifanyika kwa utaratibu unaofaa.
Alikuwa na nafasi ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, alisikilizwa wakati wa mchakato, na rufaa yake ilikataliwa kwa kukosa mashiko.
“Mshtakiwa (Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Murang’a) kwa kutumia ushahidi ulio thabiti, amethibitisha kwa mizani ya uwezekano kuwa mlalamishi alikuwa na uhusiano usiofaa na mwanafunzi, kinyume na kanuni za maadili za taasisi hiyo,” alihitimisha Jaji Nduma.