Mwenyekiti wa Supkem Hassan Naado achunguzwa kwa dai alifyatulia waandamanaji risasi
MWENYEKITI wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (Supkem), Hassan Ole Naado, anachunguzwa kufuatia video ya CCTV iliyosambazwa ikimuonyesha akichomoa bunduki na kufyatua risasi kuelekea waandamanaji.
Katika video hiyo, Bw Ole Naado anadaiwa kuonekana akielekeza silaha kwa kundi la waandamanaji na kufyatua risasi akijaribu kuwatawanya nje ya makao makuu ya Supkem jijini Nairobi mnamo Oktoba 24, 2025.
Taifa Leo imebaini kuwa uchunguzi unaendelea katika Kituo cha Polisi cha Central, ambako tayari Bw Ole Naado amerekodi taarifa.
Katika mahojiano ya kipekee, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kaunti Ndogo (DCIO) katika kituo hicho alithibitisha kuwa watu watatu tayari wamerekodi taarifa na bunduki inayodaiwa kutumika katika tukio hilo imetwaliwa.
“Kesi inaendelea kuchunguzwa. Tumeita watu kadhaa kuja kurekodi taarifa,” alisema DCIO huyo.
Kulingana na afisa huyo, bunduki iliyotwaliwa inaaminiwa kuwa ya mmiliki aliye na leseni na itafanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.
Miongoni mwa waliorekodi taarifa ni Mkurugenzi Mkuu wa Kitaifa wa Supkem Lattif Shaban, ambaye amekuwa akiongoza wito wa kufanyika kwa uchaguzi mpya na mabadiliko ya uongozi.
Bw Lattif aliambia Taifa Leo kuwa aliitwa kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Supkem akidaiwa kuwa miongoni mwa waliopanga maandamano hayo.
Barua ya DCI iliyoonwa na Taifa Leo inasema: “Ninakuita ufike katika Ofisi ya DCI Central, Nairobi, Ofisi Nambari 28, Alhamisi 20/11/25. Makosa ni kusababisha vurugu kwa njia inayoweza kuvuruga amani na uharibifu mbaya wa mali. Mlalamishi ni Hassan Ole Naado na wengine.”
Hata hivyo, Bw Lattif alisema “kosa lake” pekee lilikuwa kulaani vikali kitendo cha kufyatulia risasi vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani.
“Waliuliza kwa nini nilihutubia wanahabari Nairobi. Nikawaambia nilizungumza kama Mkurugenzi Mkuu aliyechaguliwa kihalali mwaka 2017. Huo ni ukweli — hatujawahi kufanya uchaguzi mwingine tangu 2017,” alisema.
Alisisitiza kuwa hataogopa kuendelea kuitisha uchaguzi mpya na akakana madai kwamba aliwalipia waandamanaji.
“Ninaishi Nyeri. Sijui wametumia nini kudai nililipa wahuni, watu waliandamana kwa sababu ya uchaguzi, si vingine,” alisema.
Mwanachama mwingine wa baraza, Hussein Adan Somo, pia ametakiwa kufika mbele ya wachunguzi kutoa taarifa.