Rais ahimiza wanawake kujitajirisha kutokana na mipango ya serikali
RAIS William Ruto amewahimiza wanawake wa Kenya kutumia ipasavyo mipango ya serikali ya uwezeshaji inayolenga kuwaimarisha kiuchumi.
Rais alisema baadhi ya mipango ya serikali, ikiwemo Hazina ya Hustler Fund, zinafanana sana na mbinu zinazotumiwa na vikundi vya wanawake katika maeneo mbalimbali nchini.
“Nataka niwaambie wanawake ambao wana akiba katika vikundi kwamba wanaweza pia kukopa kutoka Hustler Fund kwa sababu inatoza riba ya chini na ina masharti nafuu,” alisema.
Alitoa kauli hiyo alipohudhuria sherehe za kuadhimisha miaka 16 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Joyful Women Organisation (JoyWo), ambalo mlezi wake ni Mama Taifa Rachel Ruto.
Waliohudhuria ni pamoja na Mama Rachel, Waziri wa Afya Aden Duale, Waziri wa Utalii na Sekta ya Ukarimu wa Zimbabwe Barbara Rwodzi, na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Commercial Bank Annastacia Kimtai na makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali.
Rais Ruto alifichua kuwa mtindo wa biashara wa JoyWo uliongoza kuundwa kwa Hazina ya Hustler Fund, ambayo alianzisha alipotwaa uongozi mwaka 2022.
Rais alisema alipokuwa mbunge, alijaribu mara kadhaa kuanzisha mpango wa kuwawezesha wanawake lakini akashindwa hadi Mama Rachel alipoanzisha JoyWo mwaka 2009.
“Ninasimama hapa nikiwa na fahari kusema kuwa kile kilichoanza kidogo kule Kamagut, Eldoret, leo kimekuwa harakati ya kitaifa katika kaunti 44 na wanachama 250,000,” alisema.
Kwa upande wake, Mama Rachel alisema tangu kuanzishwa kwake, JoyWo imesaidia kuanzisha zaidi ya biashara 300,000 na kugusa maisha ya zaidi ya watu milioni tatu.
Aidha, alisema zaidi ya Sh4 bilioni zimekopeshwa kupitia vyama katika kaunti 44, matangi 50,000 ya kuhifadhi maji yamesambazwa kwa familia mbalimbali, na miti milioni 50 imepandwa, asilimia 70 ikiwa miti ya matunda.
“Hizi si takwimu tu. Haya ni mafanikio—hatua za mabadiliko, hatua za ujasiri, hatua za wanawake wanaokataa kubaki bila kutambuliwa,” alisema.
Mama Taifa aliendelea: “Hii ndiyo maana JoyWo sio mradi. Ni undugu wa wanawake wenye ujasiri na matumaini. Na tumeona hilo katika simulizi nyingi za mafanikio.”
Alisema shirika hilo sasa linajiandaa kuingia katika mfumo wa kidijitali ili kufikia wanawake wengi zaidi wanaohitaji msaada.