Koome adumisha majaji watakaosikiliza kesi ya Gachagua
JAJI Mkuu Martha Koome amedumisha jopo la majaji walioteuliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kusikiliza kesi zinazopinga kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Kupitia taarifa rasmi, Jaji Koome alimteua Jaji Eric Ogola kuwa mwenyekiti wa jopo hilo, akishirikiana na Majaji Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi. Kesi hizo zitatajwa Mei 29 kwa mwelekeo.
“Mheshimiwa Jaji Mkuu ameteua jopo la majaji wafuatao kusikiliza kesi hizi: Mheshimiwa Jaji E Ogola (mwenyekiti), Mheshimiwa Jaji A. Mrima na Mheshimiwa Jaji Dkt F Mugambi,” ilieleza notisi kwa mawakili.
Bw Gachagua alipinga uteuzi wa majaji hao uliofanywa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, akidai kuwa mamlaka ya kuteua majaji ni ya Jaji Mkuu pekee.
Mnamo Mei 9, Majaji Daniel Musinga, Mumbi Ngugi na Francis Tuiyott wa Mahakama ya Rufaa walikubaliana naye, wakisema kuteua majaji ni jukumu la kikatiba la Jaji Mkuu na haliwezi kuhamishiwa Naibu Jaji Mkuu.
“Ni lazima tukumbuke kuwa wajibu wa kuteua jopo la majaji umetwikwa Jaji Mkuu, na hatuamini kwamba hilo ni mojawapo ya majukumu ya kiutawala yanayoweza kuhamishwa kwa Naibu Jaji Mkuu chini ya kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Huduma za Mahakama,” walisema majaji hao.
Jaji Koome alikuwa tayari ameunda jopo hilo hilo kushughulikia kesi tatu zilizowasilishwa kabla ya Gachagua kufurushwa rasmi na Seneti.
Baada ya Seneti kuthibitisha mashitaka dhidi ya Bw Gachagua na kumtimua, kesi zaidi ziliwasilishwa, zikiwemo mbili zilizowasilishwa Mahakama Kuu ya Kerugoya, ambako Jaji Richard Mwongo alitoa agizo la kusitisha mchakato wa kumteua mrithi wake hadi uamuzi zaidi utolewe.
Jaji Mwongo alihamisha faili kwa Jaji Mkuu kuunda jopo, akibainisha kuwa masuala yaliyowasilishwa yalikuwa ya kisheria kwa kiwango kikubwa na yalihitaji kuamuliwa na zaidi ya jaji mmoja.
Hata hivyo, Naibu Jaji Mkuu aliteua jopo hilo Oktoba 18 2024 na kuyakabidhi faili pamoja na kesi nyingine kutoka Nairobi jambo ambalo lilizua upinzani kutoka kwa timu ya Gachagua.
Kupitia Wakili Paul Muite, Bw Gachagua alipinga mamlaka ya Naibu Jaji Mkuu kuteua majaji wa kusikiliza kesi hizo.
Majaji Ogola, Mrima na Mugambi walitupilia mbali hoja hizo, wakisema kuwa uteuzi wa majaji chini ya Kifungu cha 165(4) cha Katiba ni jukumu la kiutawala ambalo Naibu Jaji Mkuu anaweza kutekeleza kwa niaba ya Jaji Mkuu.
Hata hivyo, Bw Gachagua hakuridhika na uamuzi huo na akaelekea Mahakama ya Rufaa, ambayo iliunga mkono msimamo wake kwamba Naibu Jaji Mkuu hana mamlaka hayo.
“Ni Jaji Mkuu pekee, na yeye peke yake, ndiye anaweza kuamua idadi ya majaji wa kuteuliwa katika kesi. Vilevile, ni Jaji Mkuu pekee anayeweza kuamua majaji watakaoketi katika jopo hilo,” walisema majaji wa Rufaa.