Habari

Mwanachuo ashtakiwa kuuza karatasi feki za KCSE

Na RICHARD MUNGUTI October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Meru ameshtakiwa kwa kuuza karatasi bandia za mtihani wa kidato cha nne (KCSE) mwaka 2025.

Nasiuma Chrispinus Nambafu, mwenye umri wa miaka 22, alishtakiwa katika Mahakama ya Milimani.

Nambafu alifika mbele ya Hakimu Benmark Ekhubi ambapo alikana mashtaka matano ya kuchapisha habari za uongo, kumiliki vifaa vya mtihani bandia vinavyodaiwa kutoka kwa Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC), na kumiliki vitambulisho vya kitaifa vya watu wengine kinyume cha sheria.

Kulingana na karatasi ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kiongozi wa mashtaka Sonia Njoki, Nambafu alishtakiwa kwamba kati ya mwaka 2022 na Oktoba 11, 2025, alidai kuchapisha taarifa za uongo na kupotosha kupitia kundi la WhatsApp lililoitwa “Teachers KNEC Exams 2025”, akidai kwamba alikuwa na mitihani halali ya KCSE kutoka kwa KNEC.

Katika mashtaka mengine matatu, Nambafu anakabiliwa na tuhuma za kupatikana na vitambulisho vya utaifa vya Lucy Muthoni Kimencu, Bosco Kioko Wambua, na Doris Kathini Kimencu, bila ruhusa ya kisheria, katika eneo la Kianjai, Kata ya Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru.

Anadaiwa kupatikana na vitambulisho hivyo vya utaifa katika nyumba yake mnamo Oktoba 11, 2025, wakati maafisa wa DCI walipomkamata.

Mwanafunzi huyo aliiambia mahakama kuwa alikamilisha masomo katika Chuo Kikuu cha Meru cha Sayansi na Teknolojia (MUST) katika masomo ya Hisabati na Kemia na alikana mashtaka yote, akiomba mahakama impe dhamana inayofaa, akisema yeye anatoka katika familia maskini.

Hakimu Ekhubi aliwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 na wadhamini wawili wa kiasi sawa.Kesi hii itatajwa tena Novemba, 15 2025.