Wetang’ula aeleza wasiwasi kuhusu changamoto ibuka za uhamiaji
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, ameeleza wasiwasi kuhusu changamoto za sasa za uhamiaji zinazoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani, yakiwemo majimbo kama Minnesota nchini Amerika.
Akitambua kuwa Kenya na Ujerumani zina historia ndefu ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia unaojengwa juu ya heshima ya pande zote na ushirikiano wa maendeleo unaoendelea kuimarika Bw Wetang’ula ameomba Ujerumani itumie kwa nguvu sauti yake yenye ushawishi ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) kuhimiza majibu yaliyoratibiwa, yenye utu na endelevu kuhusu masuala ya uhamiaji barani Ulaya na kwingineko, kwa maslahi ya utulivu na mpangilio wa dunia.
Spika alikuwa akizungumza wakati wa mkutano na wanachama wa Kamati ya Masuala ya Kigeni kutoka Bunge la Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, uliofanyika katika Majengo ya Bunge, ukiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi Derya Turk-Nachbaur.
Spika huyo aliitaka kamati hiyo kupatia kipaumbele masuala ya dharura yanayoathiri amani na uthabiti wa dunia. Alisema masuala muhimu ya kimataifa yanahitaji kujadiliwa, yakiwemo wajibu muhimu wa mabunge katika kuunda sera za mbele za uhamiaji zinazolenga kurejesha amani, uthabiti na mpangilio wa kimataifa.
“Kenya na Ujerumani zinapaswa kuharakisha utekelezaji kamili wa Mkataba wa Ushirikiano wa Kina wa Uhamiaji ulioanza kutekelezwa rasmi Septemba 2024,” alisema Spika Wetang’ula.
Alibainisha kuwa mfumo huo ni muhimu katika kuwezesha fursa za ajira zilizoandaliwa vyema kwa wataalamu Wakenya wenye ujuzi nchini Ujerumani, huku ukishughulikia mahitaji ya soko la ajira kwa manufaa ya pande zote mbili.
Bw Wetang’ula alisisitiza umuhimu wa kuimarisha diplomasia ya bunge kati ya Kenya na Ujerumani, hatua ambayo alisema itaongeza ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu kama elimu, teknolojia, kilimo, usalama na biashara.
Aliongeza kuwa hilo litaimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili na wa kimataifa, na kuendeleza malengo ya pamoja ya maendeleo.
“Kinachoendelea Amerika ni kinyume kabisa na ubinadamu. Watu waliovaa kofia na kujificha nyuso wanaingia majumbani mwa watu na kuwafukuza bila hata kujali kujua kama ni raia au la. Serikali inafunga milango kwa wahamiaji ilhali Amerika yenyewe ni taifa la wahamiaji,” alisema Spika Wetang’ula.
Aliongeza kuwa Ujerumani inapaswa kujitokeza na kuzungumza wazi. “Kama mwanachama wa Muungano wa Ulaya, mna utajiri, uzoefu na mna uwezo wa kufanya kazi kwa njia iliyoratibiwa,” alisema.
Spika huyo pia alisema kinachoendelea Palestina hakiwezi kufikirika. “Tulaani yanayoendelea huko; kwa hakika ni mauaji ya kijamii. Makosa mawili hayafanyi jambo kuwa sahihi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Bi Derya Turk-Nachbaur, alisema Kenya inaendelea kuwa nguzo muhimu ya kiuchumi katika eneo la Afrika Mashariki na ina mchango mkubwa katika kudumisha uthabiti wa kikanda.
“Kenya ina mfumo thabiti wa kikatiba na taasisi imara kama Bunge lake,” alisema. Aliongeza kuwa ikilinganishwa na nchi jirani, Kenya imepiga hatua kubwa katika ugatuzi, utawala wa kikatiba na ukomavu wa kisiasa.